LIVE STREAM ADS

Header Ads

KITUO CHA EAGT LUMALA CHATOA ZAWADI ZA CHRISTMAS KWA WATOTO WA KAYA MASKINI ILEMELA.

Mchungaji wa kanisa la EAGT Lumala  Dkt. Daniel Kulola ( kulia), akimkabidhi zawadi ya nguo kwa ajili ya sikukuu ya krismasi mmoja wa watoto kutoka kaya masikini. 
Picha na Judith Ferdinand.
Judith Ferdinand, Mwanza
WATOTO 234 kutoka kaya maskini wilaya ya Ilemela mkoani hapa, wamepewa zawadi za nguo kwa ajili ya kusherekeha sikukuu ya Krismas na kituo cha EAGT Lumala Student.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi zawadi hizo, Mchungaji  wa kanisa la EAGT Lumala ambaye ndiye mwanzilishi wa kituo hicho, Dkt. Daniel Kulola alisema, anafurahi kuona watoto hao  wamepatiwa  nguo kwa ajili ya sikukuu kwani watajiona wako sawa na wengine kutoka kaya zenye kujiweza.

Mkurugenzi wa kituo hicho Joram Samwel alisema zawadi hizo zimegharimu sh.5.8 milion, hivyo anayofuraha kuona watoto pamoja na wazazi, wamezifurahia  na kuzipokea.

Swamwel alisema tangu kianzishwe kituo hicho maalumu kwa kuwasaidia watoto kutoka kaya maskini, kimekuwa kikitoa zawadi ya nguo kila ifikapo msimu wa sikukuu ya krismasi.
Pia alisema, mbali na kutoa zawadi hizo, wamekuwa wakiendelea kuwahudumia watoto hao katika masuala mbalimbali ikiwemo elimu.

Hata hivyo aliwaomba wazazi  waendelee kuwahudumia watoto wao kwa kushirikiana na kituo ili waweze kufikia na kufanikisha ndoto zao kimaisha.
Kwa upande wake mmoja wa watoto wanaohudumiwa na kituo hicho Joseph Mashilanga alisema, anajisikia furaha kupatiwa zawadi pamoja na huduma mbalimbali  ikiwemo elimu, kwani   wazazi wake hawana uwezo wa kumtimizia mahitaji , kutokana na kipato duni.

Pia aliiomba serikali ianzishe vituo kama hicho sambamba na mashirika mbalimbali yaendelee kuwahudumia na kuwasaidia watoto wanaotoka katika familia masikini, ili waweze kufikia ndoto zao.

Naye mmoja wa wazazi  wa watoto hao Maria Samson,  alimpongeza Dkt.Kulola kwa kuanzisha kituo hicho, kwani kimewasaidia katika masuala mbalimbali ya kuwahudumia watoto kama elimu pamoja na kuwapatia nguo kwa ajili ya kusherekeha sikukuu, jambo ambalo ni faraja kwa familia zenye kipato duni.

No comments:

Powered by Blogger.