NI HEKIMA PEKEE: SERIKALI IMALIZE TATIZO LA WATOTO WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA HATARISHI.
Na Judith Ferdinand, Mwanza
SERIKALI imetakiwa kuweka mikakati ya pamoja na taasisi binafsi zinazohusika na masuala ya utetezi wa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, ili kutatua changamoto zinazowakabiri watoto wanaoishi katika mazingira hayo na hatimae kumaliza tatizo hilo.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Ni Hekima Pekee, Onesmo Kajuna, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hili ofisini kwake.
Alisema mikakati itakayowekwa na serikali iwe endelevu kwa kuitazama changamoto hiyo kwa kina, ikiwa ni pamoja na kufanya kazi na familia husika bila ya kutumia nguvu.
Kajuna alisema, changamoto kubwa inayoyosababisha watoto kuishi katika mazingira hatarishi ni umaskini, kutoelewana kwa wazazi, vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa, hivyo wanaona bora kukimbilia mtaani wanakoisi kuwa ni salama kumbe siyo.
Pia alisema, ili kukabiliana na changamoto hiyo, serikali na taasisi binafsi inatakiwa kuziwezesha familia maskini kwa kuwapatia elimu kuhusu ujasiriamali sambamba fedha za kuanzisha biashara.
Hata hivyo aliiomba serikali, ianzishe vituo maalumu vya kutoa ushauri nasaha juu ya malezi ya mtoto na ndoa, ili kukomesha ongezeko la watoto waishio katika mazingira hatarishi.
Aliitaka jamii, kuendelea kushirikiana na serikali katika kutetea na kuwasimamia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa kuwafichua wale wanaowafanyia vitendo vya kikatili, ili kupunguza changamoto hiyo.
Kadhalika, serikali na taasisi zinazohusika na masuala ya haki za watoto zichukue hatua za kisheria na kuwafuatilia wale wote wanaowafanyia vitendo vya kikatili.
No comments: