LIVE STREAM ADS

Header Ads

MKUU WA WILAYA YA KINONDONI, PAUL MAKONDA AISHUKURU TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE

DC. Paul Makonda
Mnamo tarehe 23 wilaya yangu iliamua kufanya upimaji wa bure wa magonjwa ya moyo, upimaji ambao niliamini ungebeba faida kubwa nne: moja, kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara miongoni mwa wananchi, pili kubaini watu ambao tayari wanasumbuliwa na magonjwa ya moyo, tatu kuchukua hatua za awali za kuwasaidia wale ambao tayari wameshashambuliwa na magonjwa hayo na mwisho kutoa elimu juu ya namna ya kujikinga dhidi ya magonjwa yote ya moyo. 

Ugonjwa wa moyo ni ugonjwa unaoweza kuzalisha magonjwa mengi sana na kama hujafanya vipimo sahihi ni rahisi kushughulika na matokeo ya ugonjwa huku ukiacha chanzo kikizaa magonjwa mengine. Mathalani, unaweza kujikuta unahangaika na kuvimba kwa miguu au kuhangaika na macho ama figo aukisukari na hata kupoteza nguvu za kiume ukifikiri ndio tatizo kumbe tatizo la msingi ni moyo. 

Kimsingi ni kwasababu hizo nilizozianisha nilichukua hatua ya kukiomba taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete kinachosimamiwa na Profesa Janabikinisaidie kutoa huduma hiyo bure ndani ya wilaya yangu.

Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza sana madaktari kutoka taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete pamoja na mwananyamala kwa kuitikia wito na kushiriki kikamilifu kulifanya zoezi hilo. zoezi ambalo lilikuwa kubwa na zito kwani kwa makadirio ya awali tulitegemea kupata watu wasiozidi 2000 ila badala yake walijitokeza wananchi zaidi ya 7000 ila kutokana na umahiri wa madaktari hao tuliweza kuhudumia zaidi ya wananchi 5900 ingawa tulilazimika kulifanya zoezi hilo kwa siku ya pili yake ambayo ilikuwa ni tarehe 24. 

Na kwa watu wengine zaidi ya 1200 waliokuwa wamebaki, zoezi lao tulilipanga na kulifanya tarehe 30 ya mwezi huu huu wa kwanza. Ukweli ni kwamba, mambo mengi yalijitokeza kwa siku hizi tatu za upimaji; wapo waliolazimika kukimbizwa kwa ambulance kuelekea hospitali za mwananyamala na muhimbili, wapo waliolazimika kupewa appointments za kuwaona madaktari, wapo waliopewa ushauri wa matumizi ya dawa na wengine kubadilishiwa dawa sambamba na maelekezo ya utumiaji wa chakula na ufanyaji wa mazoeziili kupunguza uzito. 

Nichukue tu fursa hii kuwapongeza wanakinondoni kwa kuitikia wito na kuniamini mkuu wao wa wilaya na serikali yangu kwa ujumla kwamba tuna nia njema na tunawapenda wananchi wetu kwa kuwahakikishia afya zao zinastawi na kuendelea kuwa bora siku zote. 

Kutokama na maelezo niliyoyatoa hapo juu sambamba na sababu zilizonisukuma kufanya zoezi hilo na kutokana na muitikio mkubwa wa wananchi bila kusahau matokeo ya vipimo vilivyofanyika na kupata majibu ya kwamba watu wengi wanahitaji matibabu, kubadilishiwa dawa, maelekezo ya matumizi sahihi ya vyakula pamoja na mazoezi nimefanya uamuzi wa kulifanya zoezi hili la kudumu na tayari nimeshafanya mazungumzo na hospitali kubwa na nimetafuta njia na utaratibu bora zaidi wa kulifanya zoezi hili kuwa ni zoezi la kudumu.

Sasa basi, natamka rasmi kuwa serikali ya wilaya ya kinondoni inaanza utaratibu wa kupima bure mara tatu kwa mwaka, utaratibu ambao utaanza katikati ya mwezi wa nne. Zoezi hili litafanyika kwa kupima zaidi ya magonjwa kumi ikiwemo yafuatayo: moyo, kisukari, kansa, macho, figo, meno, kifua kikuu (TB), typhoid, magonjwa ya ngozi, presha, animonia, kansa ya kizazi, kansa ya matiti, mabusha na matende. 

Kama nilivyosema hapo awali ya kwamba, nimeshafanya mazungumzo na hospitali kubwa na kila hospitali itatoa vitengo viwili au vitatu na utaratibu utakuwa hivi. Kwa mfano, utakuta banda limeandikwa Jakaya Kikwete Cardiac Institute ndani ya banda hilo utakuta madaktari waliobobea kwenye upande wa moyo na upimaji wa presha kwahiyo mtu anayetaka kupima moyo ama presha atakwenda moja kwa moja kwenye banda husika. 

Ama unaingia kwenye banda limeandikwa Ocean Road hospital kwahiyo yeyote anayetaka kupima kansa ataingia humo…hivyo hivyo kwa magonjwa mengine yote: kutakuwa na mabanda tofauti yaliyoandikwa ni hospitali gani na wanapima magonjwa gani, lengo ikiwa ni kumpa urahisi mpimaji atakayejitokeza. 

Mwisho ila si kwa umuhimu niwashukuru sana wananchi wote wa wilaya nyingine na wale waliotoka mikoa mbalimbali ikiwemo Tanga, Pwani, Morogoro, Lindi na Dodomakwa imani yao kubwa juu ya tukio hili iliyowafanya kutoka mbali na kujisogeza mpaka viwanja vya leaders wakiwa na imani ya kupatiwa huduma hata kama zoezi hili lilikuwa limewalenga wakazi wa wilaya ya Kinondoni. 

Sambamba na kuwashukuru wananchi niwashukuru pia waandishi wa habari ambao wamekuwa mstari mbele kulitangaza tukio na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa kwa wakati. 
Imetolewa na:- Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda.

No comments:

Powered by Blogger.