LIVE STREAM ADS

Header Ads

WAALIMU KATIKA WILAYA YA MAGU MKOANI MWANZA WAPEWA TAHADHARI.

Na Judith Ferdinand , Magu
Waalimu  wa shule zilizopo  katika Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza, wameagizwa kurejea katika nyumba  walizopewa na serikali kabla ya hatua za kinidhamu na kisheria kuchukuliwa.

Hii ni  kutokana na wajumbe wa baraza la Madiwani,  kutaka kufahamu watumishi wa serikali katika wilaya hiyo, lini watarejea katika maeneo yao ya kazi licha ya Mkurugenzi  Ntinika Paulo,  kutoa agizo Desemba mwaka jana la siku 14  wawe wamehamia  lakini mpaka sasa hakuna aliyetekeleza agizo hilo.

Agizo hilo lilitolewa jana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo  ambaye ni Diwani wa Kata ya Nyanguge,  Elisha  Hilali,  katika kikao cha kwanza cha baraza la madiwani.
Hilali alisema,  watumishi kukimbia  nyumba walizo pangiwa na serikali ni  kulisababishia taifa hasara, hivyo aliwataka kurejea katika makazi hayo kabla ya hatua za kisheria  chukuliwa.

“Natoa  agizo kwa  watumishi wote wakiwemo walimu waliokimbia kuishi katika  nyumba za serikali, wafanye haraka kurejea katika makazi hayo kabla ya  hatua za kisheria hazijafuatwa  kwa atakaye kiuka, kwani ni kulisababishia taifa hasara hali inayo kinzana na malengo ya Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. John Magufuli,” alisema Hilali.
Pia alisema walimu kukaa katika nyumba walizo pangiwa zitawasaidia kufanya kazi kwa ufanisi  na kuepuka kuchelewa, hali inayopingwa na Rais  John Magufuli  sambamba na kwenda na kasi pamoja na   kauli mbiu yake ya “Hapa kazi tu”.

Aidha alimuomba Mkurugenzi na Ofisa Utumishi wa halmashauri hiyo kufuatilia na kuhakikisha watumishi ( walimu) waliokimbia nyumba, wanarejea katika makazi hayo.
Pia alisisitiza watumishi wa halmashahuri hiyo kuwa na mawasiliano baina yao, yatakayo wafanya warahisishe utendaji  kazi   haraka kwa kupeana taarifa  ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Kwa upande wake Ofisa Utumishi na Utawala wa wilaya hiyo Omary Mkangama alisema,  viongozi wa ngazi ya kata, kijiji na kitongoji wanatakiwa kuhakikisha watumishi katika maeneo yao wanaishi katika nyumba walizopangiwa na serikali na kutoa taarifa endapo kutakuwa na ukiukwaji, ili taratibu za kisheria zifuatwe.


Hata hivyo Mkingima alisema,  ili kutatua tatizo la watumishi kukimbia nyumba na kwenda mjini, ameiomba serikali na wananchi kushirikiana kufanya marekebisho na kuboresha makazi hayo.

No comments:

Powered by Blogger.