WAHUSISHWA NA DAKTARI FEKI ALIEKAMATWA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA MWANZA.
Na:George Binagi-GB Pazzo
Mtu
mmoja ambae anasadikika kuwa ni daktari feki, amekamatwa katika Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekour Toure, baada ya kujifanya kuwa ni daktari wa
Hospitali hiyo kwa takribani kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Mtu huyo ambae alitambulika kwa jina la David
Igwesa, alikamatwa jana baada ya Uongozi wa hospitali hiyo kupokea
malalamiko kutoka kwa mmoja wa wagonjwa hospitalini hapo, kuwa ameombwa rushwa
kiasi cha shilingi Laki Moja na elfu sabini (170,000) ili aweze kupatiwa
matibabu.
Baada ya taarifa hiyo, uchunguzi ulifanyika na
hatimae mtu huyo akaweza kutiwa mbaroni ambapo katika kujitetea kwake amesema
kuwa ana ndoto za kuwa daktari hivyo alifika hospitalini hapo kwa ajili ya
kupata ujuzi zaidi huku akikana madai ya kuwaomba rushwa wagonjwa.
Inadaiwa kuwa daktari huyo feki alikuwa
mwanafunzi wa Chuo cha Kikuu cha Bugando ambapo katika utetezi wake, aliwahusisha
baadhi ya watumishi wa hospitali ya Sekour Toure ambao amebainisha kuwa alikuwa
akishirikiana nao, madai ambayo Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Bahati
Msaki amesema kuwa yatachunguzwa kwa ajili ya hatua za kisheria kuchukuliwa
dhidi ya watumishi hao.
Kukamatwa kwa daktari huyo feki katika Hospitali
hiyo ya Rufaa Sekour Toure Mkoani Mwanza, kunaibua hisia za wasiwasi kutoka kwa
baadhi ya wagonjwa hospitalini hapo kutokana na uwezekano wa kupata matibabu
yasiyo sahihi suala ambalo linaweza kuhatarisha zaidi maisha yao.
Nae Katibu wa Hospital hiyo Daniel Temba aliwahizima
wananchi wanaofika hospitalini hapo kupata matibabu, kuhakikisha wanaomba
risiti pindi wanapofanya malipo ya dawa ama matibabu yao.
No comments: