MGANGA WA JADI MKOANI SHINYANGA AUAWA NA MTEJA WAKE WAKATI AKIMTIBU.
Na:Shaban Njia
JESHI la Polisi Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga, linamshikilia kijana mmoja anayedaiwa kuwa mgonjwa wa akili kwa tuhuma za kumuua mganga wake wa kienyeji aliyekuwa akimnywesha dawa kwa nguvu katika Kijiji cha Ididi Kata ya Nyamilangano wilayani Kahama.
Kwa mjibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga,Mika Nyange,alisema tukio hilo lilitokea juzi baada ya Mganga huyo,Jilumba Mabula {70},kuuawa akiwa katika harakati za kumnywesha dawa,mgonjwa wake huyo,Shibo Joel{20}.
Kamanda Nyange alisema Joel ambaye ni mkazi wa Kwimba Mkoani Mwanza alifikishwa nyumbani kwa mganga huyo na ndugu zake akisumbuliwa na maradhi ya akili na ugonjwa wa kifafa ambapo alipoanza kupewa dawa aligoma kunywa huku akidai hana ugonjwa wowote.
Aliendelea kusema baada ya Joel kugoma kunywa dawa kwa madai hana ugonjwa wowote ndipo ilipomlazimu mganga huyo kuomba msaada wa watu kumshika mtuhumiwa huyo na kuanza kumnywesha kwa nguvu dawa.
Nyange alisema akiwa katika hatua hiyo Joel alifyatuka mikononi mwa watu waliokuwa wakimshikilia na kuchukua jembe la Mkono lililokuwa jirani na walipokuwa na kumpiga nalo sehemu za shavu la kulia hali iyosababisha Mganga huyo kuvunjika taya na kufariki papo hapo.
Aidha Kamanda Nyange, alisema Joel anashikiliwa na Polisi mjini Kahama katika mahabusu maalumu, kutokana na kuhisi anatatizo la akili ambapo kwa mujibu wa sheria ugonjwa wake huo utathibitishwa na daktari baada ya kufikishwa mahakamani .
No comments: