LIVE STREAM ADS

Header Ads

PUMZIKA KWA AMANI MPAMBANAJI "NG'OHI OMAGHENA".

Kutoka Kushoto ni Mzee Maina Binagi, Chacha Binagi na rafiki wa familia ya Binagi Geban Winani walipotembelea malalo ya baba yao Mzee Binagi Maihagya (Ng'ohi Omaghena) yaliyopo Kijijini kwao Kenyamanyori, Tarime Mkoani Mara hivi karibuni.
"Babu yako alifariki dunia Mwaka 1963 akiwa na umri wa miaka 75, maana nakumbuka tuliambiwa alizaliwa mwaka 1888. Na ilidhaniwa kwamba kifo chake kilitokana na Ugonjwa wa Kisukari au tetenasi kwa sababu wakati anafariki alikuwa na jeraha (kidonda) alilolipata wakati akifanya shughuli zake za Useremala". 

Hivyo ndivyo simulizi hii ya kweli kabisa ilivyoanza kutoka kwa baba yangu mdogo aitwae Mzee Maina Maihagya Binagi, tulipotembelea yalipo malalo ya babu yangu Binagi Maihagya maarufu kwa jina la "Ng'ohi Omaghena" yaliyopo katika Mtaa wa Kenyamanyori, Halmashauri ya Mji wa Tarime Mkoani Mara ambako huko ndiko yaliko makazi ya asili ya (Ukoo) familia ya Binagi.

Si rahisi kuyajua mambo haya, lakini ni mambo mhimu sana kwa vizazi vipya katika familia mbalimbali kuyajua, hivyo mimi (George Daniel Marwa Binagi) nikiwa mjukuu wa Mzee Binagi nikaona ni vyema kuyajua maana napenda sana simulizi.

Simulizi ikaendelea, "Wazazi wake na babu yako walikuwa ni Maihagya Mwita (Baba) na Ghati Chacha (Mama) wote wakiwa ni Wakurya. Nakumbuka Maihagya alikuwa jasiri sana na kijiji (Kenyamanyori kabla ya kuwa mtaa) kilikuwa kikimtegemea kwa ajili ya ulinzi hususani wizi wa mifugo ulipokuwa ukiibuka.

Sasa siku moja wezi kutoka Kijiji cha Nyamongo walikuja kuiba mifugo katika kijiji chetu na yowe ilipopigwa baba yake na babu yako ikabidi aende kupambana na wezi hao lakini kwa bahati mbaya siku hiyo walimzidi nguvu na wakamuua kwa kumchoma mkuki.

Baada ya hapo mke wake (Ghati Chacha) alianza kuishi maisha ya ujane na ikaja njaa kali kijiji kwetu hivyo ikabidi ahamie katika Kijiji cha Kinesi (Rorya) ambapo kipindi hicho tayari alikuwa amemzaa babu yako (Binagi Maihagya) japo alipohamia huko pia alizaa watoto wengine watatu ambao walikuwa wa kike.

Waliishi huko miaka mingi hadi huyu babu yako (Binagi) alipokuwa mkubwa na kuamua kurudi katika ardhi ya nyumbani (Kijijini Kenyamanyori) ambapo alioa wanawake watatu ambao ni Nyabhisi Omoroswa, Bhoke Oghitunka na Msubhi Omoghesi na kuanzisha familia hadi pale mauti yalipowafika.

Hivyo wewe ni uzao wa Marwa Binagi. Huyu Marwa Binagi ni miongoni mwa watoto wa Binagi Maihagya (Ng'ohi Omaghena) waliotoka katika uzao wa Bhoke Oghitunka.

Labda tu usichokifahamu kuhusu huyu babu yako (Binagi Maihagya, Ng'ohi Omaghena) ni kwamba, alipenda sana elimu hadi ikafikia hatua akawa na uwezo wa kusoma na kuandika kwa kujifunza mwenyewe bila hata kwenda shuleni na ndiyo maana vijana wake nikiwemo mimi (Maina Maihagya), Profesa Lyoid Manamba, Mzee Chacha, Mzee Ryoba na Mzee Makena tulipata fursa ya kupata elimu.

Lakini pia hadi mauti yanamkuta mwaka 1963, babu yako aliacha historia ya kuwa mtu aliependa sana maendeleo na aliewapenda sana watu wote na ndiyo maana alipata nafasi ya kuchaguliwa kuwa Mwanangwa (Mtendaji Kata) kipindi hicho ikiitwa Kata ya Kebaga. 

Pia alikwa Mkulima na mfugaji hodari wa mifugo mbalimbali ikiwemo ng'ombe huku akiwa ni fundi mzuri sana wa Useremala wa kutengeneza vitanda, meza, mikwaju, viti na kila aina ya ufundi wa useremala aliujua. Hata lile jeraha nililokwambia mwanzoni lilitokana na kujikata mkononi na patasi (zana ya useremala)". Alimalizia Mzee Maina.

Hakika nikatamani simulizi iendelee lakini kimvua chepesi kilichoanza kunyesha na shughuli za pale Kijijini vikakatisha uhondo huo na baba yangu mdogo (Maina) akaahidi kunisimulia zaidi siku nyingine maana babu yangu (Binagi Maihagya, Ng'ohi Omaghena) ana watoto wengi ambao bado sijapata historia yao vyema ambao kwa hakika ndio waanzilishi wa kizazi kipya cha Familia (Ukoo) ya Binagi ambacho hata mimi nakiishi hivi sasa.
BONYEZA HAPA KUSOMA KUMBUKUMBU YA MZEE DANIEL MARWA BINAGI.
Kutoka Kushoto ni Mzee Maina Binagi, Chacha Binagi na rafiki wa familia ya Binagi Geban Winani walipotembelea malalo ya baba yao Mzee Binagi Maihagya (Ng'ohi Omaghena) yaliyopo Kijijini kwao Kenyamanyori, Tarime Mkoani Mara hivi karibuni.

No comments:

Powered by Blogger.