WATAKIWA KUPAZA SAUTI KWA NJIA YA MAOMBI ILI KUTOKOMEZA VITENDO VYA UKATILI NCHINI.
Judith Ferdinand, Mwanza
Jami imetakiwa kupaza sauti kwa njia ya kumuomba Mungu, ili kukomesha vitendo vya kikatili na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), yanayoendelea nchini licha ya serikali kuonyesha juhudi ya kutokomeza vitendo hivyo.
Wito huo ulitolewa juzi na Mkurugenzi wa Mpango wa Injili ya Uponyaji ambaye pia ni muimbaji wa nyimbo za dini, Lucy Haruni katika tamasha la kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi lililofanyika kwenye kanisa la Tanzania Assemble of God (T.A.G),lililopo Mwananchi Wilayani ya Nyamagana Mkoani Mwanza.
“ Sisi Mpango wa Injili tumeamua kupinga mauaji ya ndugu zetu albino kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kupitia maombi, ili Mungu aweze kuingilia kati na kukomesha ukatili huo, hivyo naiomba jamii kuungana nasi kupaza sauti kupitia sala,” alisema Haruni.
Haruni alisema, mauaji hayo yamepelekea taifa kuingia katika historia ya ukatili licha ya kuwa na sifa ya amani, hivyo ni jukumu la kila mmoja kukomesha jambo hilo, ili damu zao zinazomwagika zisiweze kutulilia na kusababisha matatizo kwa vizazi vijavyo.
Pia alisema, jamii inapaswa kuwa rafiki wa albino kwa kuwapatia msaada wa mafuta kwa ajili ya kuzuia mionzi ya jua inayo wasababishia saratani ya ngozi, miwani ya jua, miamvuli, nguo za mikono mirefu pamoja na ajira, ili waweze kujiinua kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi.
Hata hivyo alisema, kupitia huduma ya uimbaji atawasomesha watoto watano wenye albino kutoka kituo cha Mitindo kilichopo wilayani Misungwi mpaka elimu ya juu, jambo litakalowasaidia kujitegemea hapo baadaye.
Mmoja wa watu wenye ulemavu wa ngozi ambaye pia ni Mhasibu wa Chama cha Walemavu mkoa, Angelina Chuma anashukuru kuanzishwa kwa huduma hiyo, ila anaiomba serikali kuweka mikakati ya kuzuia mauji dhidi yao kwa walio husika kunyongwa, ili wengine wawe na hofu ya kufanya vitendo hivyo.
Naye Mchungaji wa kanisa la T.A.G Ezekiel David alisema kutokana na mauaji hayo, wanaelimisha jamii kuwa albino wameumbwa kwa mfano wa Mungu kama wengine, hivyo wasiendelee kuwafanyia vitendo hivyo kwani ni dhambi.
David aliiomba, serikali kuweka mkakati wa kudhibiti imani potofu kwa kutoa elimu juu ya watu wenye ulemavu wa ngozi mpaka shule, pia iwekeze kwa watu hao kwani wana vipaji na uwezo wa kufanya mambo kama wengine.
No comments: