LIVE STREAM ADS

Header Ads

MABULA NA WENJE WAPATA PIGO, KESI YA KUPINGA MATOKEO YA UCHAGUZI MKUU JIMBO LA NYAMAGANA.

Mbunge wa Jimbo la Nyamagana (CCM)Stanslaus Mabula.
Na Peter Fabian, Mwanza
Aliekuwa mgombea ubunge jimbo la Nyamagana Mkoani Mwanza, Ezekiel Wenje (Chadema), amepata pigo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kutupilia mbali baadhi ya maombi aliyowasilisha katika kesi ya kupinga matokeo uchaguzi Mkuu jimboni humo.

Wenje aliyekuwa mbunge wa Nyamagana awamu iliyopita, alifungua kesi namba 5/2015 akipinga matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) yaliyompa ushindi Mbunge wa sasa, Stanslaus Mabula (CCM).

Pigo hilo alilipata jana, baada ya Jaji wa Mahamakama hiyo Mhe.Kakusulo Sambo, kutupilia mbali maombi ya Wenje ya kutaka kutumia fomu ya NEC namba 21B ya matokeo ya vituo vyote 693 vya jimbo hilo ili vikaguliwe upya na upande wa utetezi.

Mabula nae alipata pigo baada ya Mahakama hiyo kutupilia mbali hoja za Mawakili wake za kuiomba Mahakama hiyo kufuta kesi ya Wenje kwa kuwa haina Mashiko, hali ambayo ilitafsiriwa tofauti na Wafuasi wa Chadema ambao walianza kushangilia kuwa Wenje kashinda kesi hiyo bila kujua kuwa hoja ya kufuta kesi ndiyo imetupiliwa mbali na kesi ya msingi ya kupinga matokeo itaendelea kusikilizwa.

Kutokana na hilo, Wafuasi wa Chadema waliokuwa nje ya Mahakama hiyo baada ya kumuona Wenje akitoka Mahakamani na kuwapa salamu za “Peoples Power”  inayotumiwa na chama hicho, bila kujua kichoamliwa, walilipuka kwa shangwe na kuanza kuandamana wakidai wameshinda kesi.

Iliwalazimu polisi kuwatawanya wafuasi hao katika maeneo ya viunga vya Mahakama pamoja na maeneo mengine ikiwemo ya barabara za Nyerere, Pamba na Mlango mmoja ili wasisababishe uvunjifu wa amani na uharibifu wa mali za wananchi waliokuwa wakiendelea na majukumu yao.

Hata hivyo kesi ya Msingi ya kupinga matokeo jimbo la Nyamagana, itaanza kusikilizwa kuanzia Jumatatu ya Wiki ijayo ya March 7,2016.
Aliekuwa Mbunge na Mgombea ubunge Jimbo la Nyamagana (Chadema) Ezekiel Wenje.

No comments:

Powered by Blogger.