NYAMANORO JIJINI MWANZA WATAKIWA KULIPA KODI.
Judith Ferdinand, Mwanza
Wananchi wa Kata ya Nyamanoro Wilaya ya Ilemela Mkoani hapa, wametakiwa kulipa kodi ya majengo, ili kumuunga mkono Rais Magufuli katika suala zima la kujitegemea kiuchumi.
Wito huo ulitolewa jana na Afisa Mtendaji wa Kata Nyamanoro Nhikilo Elias, katika mkutano na wananchi uliofanyika kwenye uwanja wa mtaa wa Nyamanoro Mashariki katani hapo.
Eliasa alisema, ni wajibu wa kila mwananchi kulipa kodi ili kuleta maendeleo ya taifa bila ya kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili, jambo linalopigwa vita na Rais Magufuli.
“Wananchi mlipe kodi za majengo kwa kujiamini ili kuleta ustawi wa maendeleo ya nchi yetu sambamba na kumuunga mkono rais Magufuli ambaye ametishiwa na wafadhili kutoka nje ya nchi kusitisha misaada, kwani Tanzania bila misaada inawezekana,”alisema Elias.
Aidha aliongeza kwa kuwataka wakazi wa kata hiyo, kulipa ushuru wa kila mwezi kwa ajili ya ukusanywaji wa taka, kwani maendeleo ya nchi ni sambamba na mazingira kuwa katika hali ya usafi.
Hata hiyo, aliwaomba wanasiasa kuacha ushabiki wa kivyama kwani kipindi cha kampeni kimepita na badala washirikiane kumuunga mkono Dkt.Magufuli ili kuleta maendeleo ya nchi kwa kutumia rasilimali zilizopo na kuondokana na hali ya utegemezi kutoka kwa wafadhili.
No comments: