SERIKALI YATEKELEZA AHADI YAKE MKOANI SIMIYU.
Kufuatia utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa kupanda miti, kutunza Mazingira na Kuhifadhi Vyanzo vya Maji, Serikali kupitia Ofisi ya
Makamu wa Raisi Muungano na Mazingira, imetekeleza ahadi yake ya kugawa miche
ya miti ya matunda Mkoani Simiyu katika Majimbo ya Uchaguzi ya Busega,
Bariadi, Itilima, Kisesa, Meatu, Maswa Mashariki na Maswa Magharibi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Raisi Mhe. Luhaga Mpina,
amechangia miti ya matunda ya maembe na machungwa ipatayo Elfu Kumi (10,000)
huku, Halmashauri na Wabunge wa Mkoa huo ,wamechangia idadi ya miche inayozidi
Elfu Kumi na Tatu (13,000).
Kwa kuanzia idadi ya miche ya miti ya matunda ipatayo Elfu
Kumi na Tatu Mia Sita Sitini na Sita,(13,666) imeshapelekwa Mkoani simiyu ikiwa
ni miti ya maembe Elfu Kumi na Tatu na Mia Tano Sitini na Sita (13,566) na
Michungwa Mia Moja (100).
Awali, Mhe. Mpina akitoa ahadi hiyo alisema, Mkoa wa Simiyu
hauna miti ya matunda ya kutosha hivyo Mkakati wa upandaji miti ya matunda
utasaidia chakula kwa familia, fedha kwa kuuza matunda na malighafi kwa viwanda
nchini na kusema kuwa miti ni Mali na miti ni uchumi.
Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais inamshukuru Mhe. Daudi Njalu
Silanga (Mb). wa Itilima, kwa kujitolea usafiri wa kusafirisha miche hiyo
kutoka Chuo cha Kilimo cha Sokoine kilichopo Mkoani Morogoro.
Idadi ya miche elfu ishirini na saba (27,000) inatarajiwa
kugawanywa katika majimbo hayo, ikiwa ni pamoja na michango ya wabunge wa
majimbo hayo.
Kupitia Mkakati huo wa Kitaifa wa kupanda miti na kuhifadhi
vyanzo vya Maji, Serikali pia imewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika
kutunza mazingira na hususan wananchi wa Simiyu kuitunza miti hiyo ya muda
mfupi, ili kuiepusha nchi na hali ya jangwa na ukame.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS. 22/04/2016
No comments: