MBUNGE JIMBO LA RORYA MKOANI MARA AKABIDHI MADAWATI KWA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI JIMBONI HUMO.
Ikiwa Una Habari, Tukio, Picha, Maoni au Tangazo, Wasiliana Na BMG Kwa Nambari za Simu 0757 432694 Au Email binagimediagroup@gmail.com
Na Peter Fabian
Mbunge wa Jimbo la Rorya Mkoa wa Mara, Lameck Airo (CCM) ametumia kiasi cha Sh milioni 51 kutengeneza madawati 1,133 ambayo yametolewa kukabiliana na changamoto za wanafunzi kukaa chini kwenye shule za msingi na sekondari katika Kata zote 21 za Jimbo hilo.
Airo kwa nyakati tofauti alitembelea kwa kushitukiza baadhi ya shule za msingi za Nyanduga (aliyosoma), Mang’ore na sekondari ya Nyanduga katika Kata ya Koryo kujionea hali halisi ya changamoto ya madawati ikiwemo shule aliyosoma aliyoipatia madawati 68 kukabiliana na upungufu huo kisha kuzungumza na walimu wote na kusikiliza kero zao mbalimbali.
Mbunge Airo ambaye ametumia kiasi cha Sh milioni 51 zikiwa ni fedha za Mfuko wa kuchochea Maendeleo ya Jimbo kutengeneza madawati na kuyagawa kwenye shule zenye upungufu mkubwa ili kuokoa wanafunzi kutoka chini ikiwa ni kuunga mkono utekelezaji wa agizo la Rais Dk John Magufuli, kuhakikisha ifikapo Julai 30 mwaka huu hakuna mwanafunzi kusoma akiwa ameka chini.
Mhe.Lameck Airo akizungumza
“Madarasa yote shule za msingi Nyanduga na Mang’ore nitatoa mifuko 100 ya saruji na kila shule itapata mifuko 50 ili kufanya ukarabati wa sakafu iliyoharibika na kuwa mashimo ili madawati tuliyowapatia yaweze kudumu kwa kuwa mashimo yaliyopo yatasababisha kuharibika haraka kutokana na wanafunzi kuyakalia na kuchezacheza ,”alisema.
Airo aliwahakikishia wakuu wa shule hizo kushughulikia upungufu wa walimu ambapo atalifikisha suala hilo kwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ili kuwezesha kupatiwa walimu kukabiliano na upungufu uliopo shule ya msingi Mang’ore wa walimu wanne na Nyanduga walimu wanane unaotokana na wingi wa wanafunzi na katika shule zingine za jimbo hilo.
“Walimu mshirikiane na Kamati za shule kuhamasisha wazazi kuhakikisha wanafunzi wanahudhulia masomo kutokana na kuwepo takwimu ambayo inaonyesha wanafunzi waliomadarasani ni nusu na watoro kuwa wako majumbani hali inayosababisha ufaulu kushuka kila mwaka katika shule zenu, rai kwa watendaji wa vijiji na Kata kuchukua hatua za haraka kuwaita wazazi na walezi watakaoshindwa kuwapeleka watoto wao shuleni kuwaeleza,”alisisitiza.
Mhe.Lameck Airo akipokea kadi kutoka kwa baadhi ya waliokuwa makada wa Chadema ambao walijiunga na CCM
Airo alipokutana na madiwani wanaotokana na CCM aliwaomba kujitolea kuwatumikia wananchi na kushirikiana naye katika kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki na kuchangia kwa hiali miradi ya maendeleo katika maeneo yao pamoja na kuwatolea taarifa kwa watu wenye kutekeleza wizi na uhalifu wa kutumia silaha kwa vyombo vya dola na viongozi wa serikali.
Mbunge alikubaliana na ombi la baadhi ya walimu wanaofundisha soka kuwapatia mipira miwili na seti mbili za jezi katika shule za msingi Nyanduga, Mang’ore na sekondari ya Nyanduka katani humo alipofanya ziara hiyo ya kukagua hali ya upungufu wa madawati na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi .
No comments: