LIVE STREAM ADS

Header Ads

TFDA YAFANYA UKAGUZI MKOANI GEITA NA KUBAINI UWEPO WA KIWANDA BUBU.

Ikiwa Una Habari, Tukio, Picha, Maoni au Tangazo, Wasiliana Na BMG Kwa Nambari za Simu 0757 432694 Au Email binagimediagroup@gmail.com

Mamlaka ya Chakula na Dawa Ofisi ya Kanda ya Ziwa imefanya ukaguzi maalumu katika miji ya Buseresere na Katoro mkoani Geita na kugundua uwepo wa kiwanda bubu cha kufungasha dawa zilizokwisha muda wa matumizi, kutengeneza lebo mpya za dawa na dawa bandia.

Akiwasilisha taarifa fupi ya ukaguzi huo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Selestine Gesimba, Mkaguzi wa Dawa wa TFDA Venance Burushi alisema kuwa kiwanda bubu hicho kilikuwa katika nyumba moja ya makazi inayodaiwa kumilikiwa na George Rwenza mkaazi wa Buseresere Wilayani Chato.

Burushi alisema kuwa walipokea taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna nyumba ambayo inahisiwa kujihusisha na kazi hiyo kinyume na sheria ndipo walipoamua kufuatilia.

“Tulifika eneo hilo na tulipo ichunguza ile nyumba tuliona hakukuwa na dalili yoyote ya mtu kuishi ndani yake. Tuliondoka eneo hilo huku tukiacha mtu maalumu wa siri wa kufuatilia nyendo za nyumba hiyo. Baada ya dakika 30 mtu yule alitupigia simu kuwa ile nyumba imefunguliwa na kuwa kuna maboksi yanatolewa na kupelekwa nyumba jirani” anaeleza Burushi.

Anaongeza kuwa waliporudi na kuingia ndani walikuta dawa nyingi ambazo zimekwisha muda wa matumizi na vifungashio vyake zenye thamani ya TZS 70, 981,000/-na uzito tani 2.

“Taarifa tulizozikuta zinaonyesha kuwa kazi hiyo amekuwa akiifanya tangu mwaka 2008 na amesambaza dawa bandia katika maeneo mbalimbali nchini hasa kanda ya ziwa. Vitabu vya ankra vinaonyesha kuwa amewahi kusambaza dawa maeneo kama Bunda, Ngara, Kibondo, Shinyanga na maeneo ya Runzewe na Mwanza. Aidha baadhi ya vituo vya afya na zahanati za shule za sekondari zimewahi kusambaziwa dawa na bw. George Lwenza” alisema.

Aidha Burushi alisema kuwa ingawa ukaguzi huo ulifanikiwa lakini walikabiliana na changamoto za taarifa kuvuja. “Ukaguzi wetu uliandaliwa kwa usiri mkubwa lakini taarifa za sisi kuwepo Geita zilianza kuvuja mara baada ya kuanza kuwashirikisha watumishi wa Halmashauri. Baadhi ya watu wakaanza kufunga maduka.” alisema.

Kwa upande wake Afisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Sungu Nespory alisema kuwa wanachukua taarifa ya ukaguzi wa TFDA kama changamoto na wataongeza jitihada za ukagauzi katika eneo la Katoro ambalo lina changamoto nyingi.

Onespory alimweleza Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita kuwa wamekuwa wakikumbana na vikwazo vingi katika kutekeleza majukumu yao kutoka kwa viongozi wa kisiasa na serikali. “Kuna mapungufu upande wetu lakini tunahaidi tutasimamia vizuri mifumo yetu ya udhibiti. Hata hivyo bajeti ya kufanya ukaguzi haitoshi na wakati mwingine tumekuwa tukiingiliwa katika kazi na viongozi. Hali hii imekuwa ikiwakatisha tamaa wakaguzi” alisema.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Selestine Gesimba aliwataka watumishi wa Halmashauri za Geita Mji na Wilaya kujitathimini kufuatia taarifa ya ukaguzi ya TFDA. “Taarifa hii sio nzuri kwetu. Yapo madhambi yamefanyika Geita. Haiwezekani watu watoke Mwanza waje kuchukua hatua. Siamini kama nyinyi hamkuwa na taarifa. Taarifa hii ya TFDA inaonesha kuwa kuna tatizo” alisema.

Gesimba aliwataka watumishi wa Halmashauri kubadirika na kuhaidi kuwachukulia hatua watumishi wote watakaoshindwa kuwajibika.“TFDA wataniletea hii taarifa rasmi na nitawataka mjieleze kwa nini hali hii imetokea. Haya madhambi yamekuwepo tangu 2008. Kwa nini TFDA iweze kuyabaini na nyinyi mshindwe? Au nyinyi ni sehemu yao” alihoji Gesimba.

Aidha Gesimba aliwataka watumishi kufanya kazi kwa uadirifu na kwa kujiamini na kuwataka kumtaarifu pale watakapokwamishwa. “Mimi sina Chama ingawa natekeleza Ilani ya CCM (Chama cha Mapinduzi). Siko tayari kuona mnaingiliwa katika kazi na wanasiasa. Msisite kunieleza kama mtu yeyote atawakwamisha katika kazi” alisema Gesimba.

No comments:

Powered by Blogger.