LIVE STREAM ADS

Header Ads

NDOTO ZA WANAFUNZI KATIKA HALMASHAURI YA MSALALA ZAZIDI KUKWAMISHWA NA MIMBA.

Ikiwa Una Habari, Tukio, Picha, Maoni au Tangazo, Wasiliana Na BMG Kwa Nambari za Simu 0757 432694 Au Email binagimediagroup@gmail.com

Shaban Njia
Wanafunzi 35 wa shule za Sekondari katika halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, wamepata ujauzito kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 hali iliyopelekea kukatiza ndoto zao za maisha katika siku za baadaye.

Ofisa maendeleo ya jamii wa halmashauri hiyo, Aliadina Peter, aliyasema hayo wakati akitoa taarifa yake kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Kiwilaya katika uwanja wa halmashauri ya mji .

Sherehe za maadhimisho hayo zilijumuisha halmashauri mbili za Msalala na Kahama mji zilifanyika zikiambatana na zawadi kwa makundi mbalimbali yakiwamo ya wajane, watoto yatima, wazee wasiojiweza pamoja na kutembelea katika hospitali ya mji wa Kahama kwa lengo la kuwafariji wagonjwa.

Peter alisema kuwa zipo changamoto nyingi zinazochangia mtoto wa kike asiweze kumaliza masomo yake na kuongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2016 wanafunzi wasichana waliofaulu kidato cha nne walikuwa ni asilimia 42 huku wavulana wakiongoza kwa kiwango cha asilimia 70.

Alisema kuwa baadhi ya changamoto zinazomfanya mtoto wa kike asiweze kufaulu masomo yake ni pamoja na umasikini uliokithili katika familia zao unaosababishwa na elimu duni na matumizi mabaya ya rasilimali za familia katika maeneo waliopo.

Pia changamoto nyingine ni kutokuwepo kwa hosteli katika shule za sekondari hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa watoto wa kike kukatishwa masomo yao huku sababu kubwa ni kupata ujauzito ambao unatokana na kutembea umbali mrefu kwenda shuleni na hivyo kusababisha kubakwa.

“ Ndugu mgeni rasmi chanzo kingine kinachosababisha watoto wa kike wanaosoma Sekondari kupata ujauzito ni kitendo cha kupanga katika nyumba za watu binafsi kwa ukosefu wa hosteli hali inayopelekea kukosa ulinzi ama usimamizi mzuri  wa wanafunzi hao,” alisema Peter.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu aliwataka Wazazi kuhakikisha wanawasimamia vizuri watoto wao waanamaliza masomo wakiwa salama pamoja na kuwaendeleza kwa masomo ya elimu ya juu na kuongeza kuwa serikali haitamvumilia mtu yeyote atakaye katiza masomo ya mwanafunzi

“Ole wake mzazi atakaye mzuia mwanafunzi aliyefaulu kidato cha nne na kujiunga na masomo ya elimu ya juu, serikali haitamvumilia mtu wa namna hiyo ikiwa ni sambamba na wale wanaowapa ujauzito wanafunzi hili ni agizo linapaswa kuzingatiwa usije jikuta upo mikononi mwa dola,” alisema mkuu wa Wilaya Fadhili Nkurlu.

Akizungumzia masuala ya Viwanda vidogo vidogo Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wanaume kutowazuia wake zao kwenda kukopa katika taasisi za fedha kwa lengo la kuanzisha viwanda hivyo ili waweze kuinua uchumi na kuleta manufaa katika familia zao.

Kaka sherehe hizo Nkurlu aliweza kutoa misaada mbalimbali kwa wazee 18 wasiojiweza, wajane 18 na mlemavu mmoja wa viungo anayetoka Kata ya Bugarama iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 1.8 ambapo kila mmoja wao alipatiwa unga wa sembe kilo kumi, mchele kilo kumi na mafuta ya kupikia lita tatu.

No comments:

Powered by Blogger.