LIVE STREAM ADS

Header Ads

MIAKA 53 YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR 2017.

Ikiwa Una Habari, Tukio, Picha, Maoni au Tangazo, Wasiliana Na BMG Kwa Nambari za Simu 0757 432694 Au Email binagimediagroup@gmail.com

Na Emmanuel J. Shilatu
Ni miaka 53 imetimia tangu jahazi lililowabeba Watanganyika na Wazanzibar liweke historia ya kung’oa nanga mara baada ya Jamhuri Muungano wa Tanzania kuzaliwa rasmi mnamo April 26,1964. 

Hii ilitokana na ujasiri, ushupavu na nia ya dhati waliyokuwa nayo waasisi wa Muungano huu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika) na Abeid Aman Karume (Zanzibar).

Hatua hiyo ilifikiwa kutokana na mtiririko wa kimazingira na mahusiano ambayo yalishabihiana kama sio kufanana kabisa kwa pande zote mbili (Tanganyika na Zanzibar). Zipo sababu za kijiografia, kisayansi, kitamaduni  na kihistoria zilizochangia huu muungano wetu.

Kutokana na sababu za kijiografia na kisayansi inaaminika kabisa kwamba Visiwa vya Zanzibar (Pemba na Unguja) vilikuwa vimeungana na hata kushikamana kwa pamoja pembezoni mwa pwani ya ardhi ya Tanganyika. Hivyo tangu awali tulikuwa ni kitu kimoja, tulio katika ardhi moja na ya pamoja.

Pia kuna historia (isiyo na shaka)  ya muingiliano wa kiutamaduni baina ya Wakazi wa Tanganyika na Zanzibar ambapo hali nzima ya kuoa ama kuolewa ilizidi kushamiri baina yao.

Halikadhalika harakati za kudai ukombozi wa uhuru wetu ili tuweze kujitawala wenyewe kutoka kwa dudu la wakoloni nazo zilichangia kutuunganisha. 

Inaaminika (na ndiyo ilivyo) ya kuwa asilimia kubwa ya Wazanzibar walishiriki kwenye harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Mwingereza ambapo kutokana na nia, ushupavu na nguvu ya pamoja walifanikiwa kupata Uhuru wa Tanganyika mnamo Desemba 9, 1961.

Lakini pia licha ya asilimia kubwa ya Wazanzibar kushiriki katika mchakato wa Mapinduzi ya Zanzibar lakini pia kulikuwepo na asilimia kubwa ya mchango wa ushiriki kutoka kwa Watanganyika. 

Hatimaye matunda yake yalionekana ya mapinduzi matukufu yaliyofikia kilele katika uwanja wa Gombani Pemba yaliyofanyika Jamhuri 12, 1964, baada ya kuchoshwa na hila na ghiliba za Waarabu uliotamalaki visiwani humo kwa zaidi ya karne mbili na hatimaye waliwaacha wazalendo watwana katika ardhi yao.

Pia tusisahau lengo na nia ya dhati aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere ya kutaka kuiunganisha Afrika mzima kwa hatua lakini jitihada zake zilianza kuzaa matunda ambayo hayatakaa yatokee tena Afrika kwa kuiunganisha Tanganyika na Zanzibar.

Mnamo April 22, 1964, Maraisi wa nchi hizi mbili ambazo sasa zinaunda Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (wa Jamhuri ya Tanganyika) na Abeid Amani Karume (wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar ) walitia sahihi Mkataba wa kimataifa wa kuunganisha nchi zao, unaojulikana kama “Hati ya Muungano” (Articles of union) na hivyo kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ama United Republic of Tanganyika and Zanzibar (URTZ) ambao ni muungano sahihi kabisa kisheria na unaotambulika Kikatiba.

Siku ya Jumatatu ya tarehe 26 Aprili, 1964 viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee kwa nia ama lengo moja tu la kubadilishana “Hati za Muungano”.

Wananchi wa Tanzania walipiga kura kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa kwanza kabisa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwaka 1965.

Kama nilivyodokeza kwamba Muungano wa Tanzania ulifikiwa kwa kutiwa sahihi mkataba unaoitwa Hati ya Muungano (Articles of the Union) na wakuu wa nchi hizi mbili, Mwalimu Nyerere (Tanganyika) na Abeid Karume (Zanzibar) Aprili 22,1964 na kuridhiwa na mabunge ya nchi hizo Aprili 25, 1964 na hatimaye kuwa sheria ya Muungano ya (Acts of Union) ya mwaka 1964.

Kimsingi sheria ya Muungano ndiyo iliyoanzisha na ndiyo iliyopewa haki ya chombo cha kikatiba kinachodhibiti katiba zote mbili za Serikali ya Muungano.

Mwanzoni kabisa Hati ya Muungano (Articles of Union) iliyomo ndani ya sheria ya Muungano iliorodhesha na hata kudadavua mambo 11 ya Muungano. 

Mambo hayo ni kama vile:- Mambo ya nchi za nje, Ulinzi na usalama (lakini si usalama wa Taifa); Polisi, Uraia, uhamiaji, mikopo na biashara za nchi za nje, utumishi katika serikali ya Muungano, kodi ya mapato, usimamizi wa fedha, Bandari, Usafiri wa anga, Posta na simu.

Kwa nia safi na malengo mazuri yanayojitokeza Hati ya Muungano imekuwa ikiboreshwa zaidi kwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele kwa malengo kusudi ya kuleta umoja, mshikamano, amani na utulivu wetu ule ule tulioanza nao awali na halikadhalika maridhiko yanayoendelea kuufanya Muungano huu uendelee kudumu hadi hii kesho.

 Ndio maana mtu timamu hatoshangaa sana kuona Hati ya Muungano ikiendelea kuboreshwa kila siku (na itaendelea hivyo) ambapo ilianzia na mambo 11 ambapo hii leo yamefikia takribani 23.

Mengineyo ama baadhi ya yale yalioongezeka ni kama vile;- Noti; Elimu ya juu,; Maliasili na mafuta (mafuta) yasiyochujwa, bidhaa za mafuta na gesi asilia , ya mwaka 1968; Baraza la Mitihani ya Taifa; utafiti; utabiri wa hali ya hewa; Takwimu,; Mahakama ya Rufaa ya juu ya mwaka 1979; pamoja na uandikishwaji wa vyama vya kisiasa .

Tusisahau mwaka 1965 iliundwa katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (The Interim Constitution of The United Republic of Tanzania) mpaka kufikia mwaka 1977 ndipo ilipoundwa katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo inaendesha nchi hadi sasa.

Mwaka huo huo wa 1977 (yaani miaka 13 baada ya Muungano kutokea) kulikuwa na muungano wa vyama vikubwa viwili kuungana kutoka pande zote mbili (Bara na Visiwani). Vyama hivyo ni TANU (Tanganyika African National Union) pamoja na ASP (Afro Shiraz Party) cha Zanzibar kuungana na kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hatua ama vitendo na mafanikio hayo si tu kwamba yalidumisha bali hata yaliendeleza kukuza Muungano wetu ambao Jahazi lake liligubikwa na misukosuko ya mawimbi makubwa baharini uliojaa uzito wa mambo mbalimbali uliokuja kwa sera ya kero zilizoleta chokochoko mbalimbali katika Muungano wetu., ambao hatutakiwi kamwe kuusahau maishani mwetu. 

Tusisahau mchezo mchafu uliojaa rafu za kutisha uliotaka kufanywa na Bunge miaka ya 1990 na 1992 ya kutaka kuyakubali madai yaliyotolewa na kundi la G55 ambalo lilitaka kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika , hali hii ingetuvuruga kwani ilihitaji uwepo na serikali tatu yaani Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakika yatupasa tuzishukuru hekima na busara za Mwalimu Nyerere kwa kutuokoa na chokochoko ya kero hii.

Pia tusiisahau kero ama chokochoko nyingine ya Muungano wetu iliyoibuka Decemba 1, 1992, ambayo Zanzibar ilitaka kujiunga na umoja wa Nchi za Kiislam Duniani (OIC) kama nchi nje ya Muungano.

Tuendelee kukumbuka ni kwa jinsi gani Zanzibar iliyokuwa inasaka ukuu nje ya Muungano kwa kuibua madai ya Bendera ya Taifa lake (Zanzibar), wimbo wa Taifa, na nembo yao ya Taifa.

Kwa nyakati tofauti tofauti tumekuwa tukisikia baadhi ya Wazanzibari walio wachache wakiilalamikia hali nzima ya ongezeko la mambo kwenye Hati Muungano (Articles of Union) kutoka mambo 11 hadi kufikia 23 ambalo ni sawa na ongezeko la mambo 12 ambao kwa baadhi yao hawaoni umuhimu wa wa uwepo wake na hata kutishia kujitoa.

Ila asilimia kubwa ya Wazanzibari wanayaunga mkono, hali iliyo sababisha hoja ya wachache kuzidiwa nguvu.
Pia tumekwisha sikia jinsi gani Wazanzibari wanavyotaka jambo la maliasili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa na aina nyingine za mafuta au bidhaa na gesi asilia iondolewe katika masuala ya Muungano ili Zanzibar ipate kunufaika zaidi na maliasili zake.

Kukuru kakara za Wazanzibari zinatookana na madai yao ya kuwa Tanganyika(Bara) imeimeza Zanzibar (Visiwani) katika masuala mazima yahusuyo Muungano.

 Ikumbukwe Ubaguzi wa dhana ya Tanganyika umeimeza Zanzibar si ya kweli na hii imebainishwa katika katiba ya Muungano kuwa kuna Serikali ya Jamhuri ya Muungano na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Haya ni mapenzi ya dhati waliyoonyesha kwa Wazanzibari kwa kuwaruhusu wawe na serikali yao ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ikumbukwe Serikali ya Muungano inaongozwa na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaongozwa na Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar na chombo chao cha kutunga sheria kinaitwa Baraza la Wawakilishi.

Ndugu zangu hali ya kupuuzia na hata kuuchezea Muungano wetu ni hatari sana tena ni dhambi iliyotukuka. Mathalani Wazanzibari wakiamua kujiengua kwenye huu Muungano ili wawe kivyao vyao,hawatabaki salama. 

Mwalimu Nyerere alishawahi kusema ya kuwa “wakifika kwenye hatua hiyo watagundua kuwa ndani yao kuna Wazanzibari na Wazanzibara”. Nao wataamua kuwafukuza wale wa Wazanzibara, lakini hiyo haitakuwa mwisho. Punde si punde watajigundua kuwa nao (Wazanzibari) wamegawanyika kwani kuna Wapemba na Waunguja, na wakifikia hapo pia hawatakuwa salama ni lazima machafuko yatatokea.

Daima Wazanzibari watambue ya kuwa dhambi ya kutokutamalaki kwa dhana ya Unguja na Pemba unatoka na kufunikwa na kivuli cha mwamvuli cha Muungano. Hivyo umoja, mshikamano, amani na utulivu wao unategemea sana uwepo wa nguzo hii imara ya Muungano huu tulionao.

Vivyo hivyo kwa watu wa Bara (Tanganyika) ni rahisi kwao kutafunwa na dhambi ile ile ya ubaguzi watakayo ianzisha nje ya uwepo wa Muungano ni rahisi sana kwa ukabila, udini, ukanda na hata U-rangi kutamalaki ndani ya jamii wakishafikia hapo, hawatabaki salama kwani watachafuana tu.

Muungano huu tulionao unawafanya wale wageni, mataifa ya nje na watu wote wenye hila, donge, roho ya korosho kuogopa kutugusa na kutuvuruga kutokana na kuwepo kwa nguvu kubwa ya umoja, ushirikiano na mshikamano baina yetu. 

Muungano huu wetu unatupatia fursa kubwa ya uhuru wa kusafiri kwa pande zote iwe ni bara ama ni visiwani. Leo hii ni rahisi sana kwa mtu wa bara kwenda Visiwani na hata wale wa Visiwani kuja Bara kwa uhuru zaidi kwani Uhuru huo wa uwepo wa nafasi hiyo umeshalipiwa na huu Muungano wetu tulionao.

Kutokana na uwepo wa uhuru wa kusafiri usio na mipaka baina yetu, pia Muungano wetu tulionao unazidi kutuongezea fursa na nafasi zaidi ya uwanja mpana wa ufanyaji biashara. Hali hii imesababisha uwepo wa mzunguko mkubwa wa pesa ndani yetu kwani si jambo la ajabu kuona pesa zikitoka Visiwani (Zanzibar) kuja Bara (Tanganyika) kupitia mabadilishano ya bidhaa kama vile nafaka, kahawa, matunda, vipuri vya magari na kadhalika.

Pia si jambo geni tena kwa sasa kuona pesa zikivuka Bahari na kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya ufanyaji ama ununuzi wa biashara kama vile Magari, nazi, Karafuu, Tende na kadhalika.

Muungano huu unatuzidishia fursa ya mianya ya uwanja mpana tena usio na kikomo wa ufanyaji biashara, Muungano huu hautubagui ama kutojulisha au kuwa na upendeleo wa upatikanaji wa Elimu bora, huduma za kijamii bora, Muungano hautugawi wala kuwa na upendeleo bali umejaa uwiano sahihi wa upatikanaji wa mabo yote ya msingi yaliyomo ndani ya “Hati ya Muungano” (Articles of union). 

Muungano huu ni nguzo imara katika muktadha mzima wa nyanja za kimaisha yetu. 

Ni ukweli uliodhahiri kuwa haitakaa itokee Muungano kama huu (wa Tanganyika na Zanzibar) hapa Barani Afrika umoja ushirikiano, ushikamano, amani na utulivu ni sehemu mojawapo ya manufaa ya Muungano huu. 

Njia mojawapo ya kuwaenzi vyema waasisi wetu ni kwa kuudumisha Muungano wetu ambao ni urithi wa aina yake waliotuachia. Watanzania yatupasa tuenzi Muungano wetu kwa kuulinda na kuudumisha kwa vitendo kwani ni nguzo na fahari ya kipekee na ya aina yake Barani Afrika.

Tuadhimishe Miaka 53 ya Muungano kwa kuudumisha, kupiga vita madawa ya kulevya na kufanya kazi kwa bidii
Endapo itatokea kiongozi yeyote Yule ama utawala wowote ule utakaokuwa na malengo ya kuubomoa ama kuuvunja Muungano huu, basi ajue dhambi hii itamtafuna yeye na kizazi chake milele.

Mungu atuepushe na mawazo ya kuuvunja Muungano huu vichwani mwa viongozi/watawala wetu, atuepushe na balaa hili lisijitokeze kwenye Katiba Mpya ijayo. Kheri ya Miaka 53 ya maadhimisho ya Muungano!!
Tuwasiliane 0767 488622  www.ndgshilatu.blogspot.com

No comments:

Powered by Blogger.