LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wachimbaji wadogo wa madini mkoani Lindi waiomba Serikali iwasaidie zana za uchimbaji

Wasiliana na BMG Blog/ BMG Online TV kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma ya Habari na Matangazo.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akifafanua jambo alipofanya ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Namungo uliopo Wilayani Ruangwa mkoani  Lindi ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na kutatua kero mbalimbali. Katikati ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Sophia Omari.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akipata maelezo kuhusiana na shughuli zinazofanywa na kampuni  inayojishughulisha na utafiti  wa madini ya Kinywe ya Ngwena Limited iliyopo Wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akizungumza na  wananchi wa kijiji cha Nangurugai kilichopo Wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
Mmoja wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika kijiji cha Namungo Wilayani Ruangwa mkoani Lindi akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akikagua shughuli za uchenjuaji wa madini ya dhahabu  katika Mgodi wa Dhahabu wa Namungo uliopo Wilayani Ruangwa mkoani  Lindi.

Na Greyson Mwase, Ruangwa
Wananchi ambao ni wachimbaji madini katika Kijiji cha Namungo kilichopo Wilayani Ruangwa mkoani Lindi, wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kuwapatia zana bora za uchimbaji ili kuboresha zaidi shughuli zao kuchangia kwenye pato la taifa kupitia sekta hiyo.

Waliyasema hayo jana Disemba 14, 2018 katika mkutano wa hadhara uliofanywa katika Kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku mbili ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo mkoani Lindi yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na kutatua kero mbalimbali.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, Dickson Baltazary ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu alisema kuwa, wamekuwa wakichimba madini kwa kutumia zana duni hali inayowasababishia kushindwa kufikia malengo yao kwenye uzalishaji.

Baltazary aliongeza kuwa, iwapo watapata fedha kupitia mikopo na ruzuku Serikalini kupitia Wizara ya Madini wataweza kufanya shughuli zao za uchimbaji wa madini kwa ufanisi na kuchangia zaidi kwenye mapato ya Serikali.

Akizungumza na wachimbaji hao mara baada ya kupokea kero mbalimbali, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia wachimbaji wadogo ambapo mpaka sasa maeneo yameanza kutengwa kwa ajili ya uchimbaji madini. Aliendelea kusema kuwa Serikali inaangalia utaratibu mzuri utakaowawezesha kupata ruzuku.

Wakati huo huo, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nangurugai Wilayani Ruangwa mkoani Lindi Naibu Waziri Nyongo aliwataka wananchi kuunga mkono uwekezaji wa uchimbaji wa madini ya kinywe (graphite) unaotarajiwa kufanya na kampuni ya utafiti wa madini hayo ya Chilalo Graphite Mine.

Aidha aliwapongeza wananchi hao kwa kuunga mkono uwekezaji huo kwa kuwa na subira wakati wa tathmini iliyofanywa miaka miwili iliyopita na kuitaka kampuni ya Chilolo kurudia tathmini kwani thamani ya mali imebadilika.

Akielezea manufaa ya mradi huo, Nyongo alieleza kuwa ni pamoja na ajira 480 kutolewa wakati wa ujenzi wa mgodi na ajira 250 kutolewa mara baada ya uendeshaji wa mgodi kuanza.

Alieleza manufaa mengine kuwa ni pamoja na kukua kwa uchumi wa Wilaya ya Ruangwa kutokana na ongezeko la mapato yatokanayo na uzalishaji wa madini hayo.

"Madini ya kinywe yana soko kubwa duniani kutokana na kampuni nyingi kutumia madini hayo katika utengenezaji wa betri za magari, ni vyema mkachangamkia fursa mbalimbali zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi". Alifafanua Nyongo.

Katika hatua nyingine, Nyongo aliutaka mgodi huo kuhakikisha unatoa ajira kwa wananchi wenye sifa wanaozunguka karibu na mgodi kabla ya kufikiria kuajiri wageni kutoka katika mikoa mingine.

No comments:

Powered by Blogger.