LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la "Voce Of Hope" lakabidhi bima kwa watoto wenye vichwa vikubwa Jijini Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Judith Ferdinand, BMG
Kutokana na changamoto ya matibabu inayowakabili watoto wenye vichwa vikubwa (vichwa maji) na mgongo wazi,  taasisi ya Voice of Hope imewakatia bima ya afya watoto kumi wenye tatizo hilo ambao wanalelewa katika Kituo cha Nyumba ya Matumaini Jijini Mwanza.

Akizungumza baada ya kukabidhi fomu za bima hizo, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Athuman Thabit alisema kwa sababu wanatambua matatizo hayo wanaanzia Mwanza na baadaye nchi nzima kuhamasisha jamii iweze kutambua walemavu wanahaki sawa ya kupata mahitaji muhimu ikiwemo huduma za afya.

Alisema wameanza na bima hizo kumi na baadaye watakua na kampeni ya kuchangia kwa hiari bima ya afya kwa watoto hao sanjari na harambee kwa Mkoa wa Mwanza na nje ya mkoa kwa ajili ya kupata fedha zitakazowezesha kila mtoto mwenye tatizo hilo kupata bima ya afya.

"Tumekuja kuwatembelea watoto waliopo katika nyumba ya matumaini, baada ya kuguswa na changamoto zinazowakabili kwani wengi wao wanafariki kutokana na kukosa matibabu ambayo ni gharama kubwa ukizingatia familia zao kwa asilimia kubwa ni maskini, hivyo tumewapa wakatia bima kumi kwa kuanzia, na katika kuhakikisha kila mtoto mwenye ulemavu huo anakuwa na bima tunatarajia kuwa na kampeni hiari ya kuchangia bima ya afya maalum kwa watoto hawa pamoja na harambee kwa Mkoa wetu wa Mwanza na nje ya mkoa". Alisema Thabit.

Kwa upande wake Meneja wa Kituo cha Nyumba ya Matumaini ( Hope House), Sifa John alisema, kwa sasa wametimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa kituo hicho wameisha hudumia watoto 359 ambapo awali lengo lao ilikuwa ni kuhudumia watoto saba kwa wiki ila wanapokea 20.

Lengo la kuanzisha kituo hicho ni kuwapatia watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi huduma ikiwemo mazoezi, kuwaunganisha wazazi na wadau mbalimbali ambao watasaidia katika matibabu pamoja na kuwapatia elimu ya namna ya kuwahudumia pamoja na jinsi ya kuzuia kuzaa watoto wa namna hiyo.

John alisema changamoto iliyopo ni jamii kutokuwa na ulewa juu ya kichwa kikubwa na mgongo wazi hivyo kuwanyanyapa, uhaba wa vifaa visaidizi kwani ni watoto wanakuwa na uzito mkubwa, wengi wanao wapokea wanakuwa na utapia mlo, hali duni inapelekea kukaa nao kituoni hapokwa muda mrefu hali inayopelekea kuwa na uhaba wa chakula.

Alisema kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano, Serikali inagharamia upasuaji huku shirika la Marafiki wa Watoto Wenye Kansa, Vichwa vikubwa na mgongo wazi likitoa mipira maalum inayotumika kuwekwa kichwani kwa ajili ya kuteremsha maji mpaka tumboni na kwa upande wa vipimo vya uchunguzi, gharama ni kwa wazazi ambayo inawapa wakati mgumu wazazi kwani wengi wao wanatoka katika familia maskini na kipato chao ni duni hivyo katika kuwasaidia kwenye jambo hilo wamekuwa wakiwaunganisha na wadau kama Taasisi ya Desk and Chair Foundation kwa msaada zaidi.

Baadhi ya wazazi wenye watoto wenye vichwa vikubwa walitoa shukrani kwa taasisi Voice of Hope kwa kuwasaidia bima hizo kwani wao kutokana na hali duni wanakosa shilingi 50,400 kwa ajili ya kuwakatia bima hivyo aliomba wadau wengine kuendelea kuwasaidia na kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo vifaa vya mazoezi.

No comments:

Powered by Blogger.