LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto wazinduliwa wilayani Kishapu

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Nyabaganga Talaba (kushoto) akipokea nyaraka za mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agape ACP, John Myola (kulia) wakati wa uzinduzi wa mradi huu. 
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto unaotekelezwa na Shirika la Agape ACP katika Kata ya Kishapu, Itilima na Bunambiyu wilayani Kishapu. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agape ACP, John Myola.
Mkuu wa Wilaya Nyabaganga, Talaba akikata utepe wakati wa uzinduzi wa mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agape ACP, John Myola akielezea lengo la mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto unaowalenga wanawake wenye umri wa miaka18-55 na watoto wenye umri wa miaka 7- 17. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Underson Mandia akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba.
Msimamizi wa mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto, Felix Ngaiza akitambulisha mradi huo.
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Joseph Swalala akiwataka Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji kutoa ushirikiano katika kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake.
Wadau wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa uzinduzi wa mradi huo.
Baadhi ya wanao waliohudhuria uzinduzi huo.
Wadau mbalimbali wakiwa ukumbini wakati wa uzinduzi wa mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto.
Wadau wakifuatilia uzinduzi huo.
Uzinduzi wa mradi huo ukiendelea.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Shinyanga, Glory Mbia akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa Sauti ya Mwanamke na mtoto wilayani Kishapu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agape ACP, John Myola akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Afisa Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza wa Mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto, Lucy Maganga akisisitiza wadau katika mradi huo kufanya kazi kwa weledi na kutokuwa waoga ili kumkomboa mwanamke na mtoto.
Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Anderson Mandia akisisitiza kuwa Madiwani wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto.
Picha ya pamoja baada ya uzinduzi wa mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto wilayani Kishapu.

Na Kadama Malunde - Malunde1 Blog
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Nyabaganga Talaba amezindua rasmi Mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto unaotekelezwa na Shirika la Agape ACP kwa lengo la kumwezesha mwanamke na mtoto kupata haki na usawa kwa wakati katika jamii.

Mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa "United Nations Development Programme- UNDP) utatekelezwa kwa kipindi cha miezi sita katika kata tatu za wilaya ya Kishapu ambazo ni Itilima,Bunambiyu na Kishapu.

Akizungumza jana wakati akizindua mradi huo katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu,Mkuu wa wilaya ya Kishapu,Nyabaganga Talaba alisema mradi huo unalenga kumuinua,kumtetea mwanamke na mtoto.

"Sauti ya mwanamke na mtoto siyo sauti ya kawaida,ni sauti ambayo ikisikika jamii hushtuka, mradi huu uwe chachu ya kuleta mabadiliko kwa wanawake na watoto, wajihisi kuwa wao ni watu wa muhimu sana katika taifa hili,tubadilike pale tulipojisahau na kusahau sauti za makundi haya,sauti, wale waliofanya wanawake na watoto wakose upendo na furaha waache sasa". Alisema Talaba na kuongeza;

"Nawashukuru UNDP kwa kuwezesha mradi huu kufanyika katika wilaya yetu,naomba wasichoke na sisi kama serikali tutahakikisha kuwa tupo bega kwa bega na Agape kuhakikisha malengo ya mradi yaliyokusudiwa yanafikia mwisho". Alisema Talaba.

Alisema hatutaweza kufikia malengo ya serikali ya kufikia uchumi wa kati kama mwanamke bado hajitambui huku akibainisha kuwa mwanamke akijitambua na taifa litajitambua lakini pia maendeleo hayaji kwa kumuacha mwanamke nyuma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agape ACP, John Myola alisema mradi huo unalenga kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora ya haki na kwa wakati muafaka miongoni mwa wanawake na watoto pamoja na kuimarisha mfumo mzima wa haki za jinai kwa upatikanaji wa haki za jinai kwa watuhumiwa na wahanga/ waathirika wa makosa ya jinai.

"Shirika la Agape ACP litashirikiana na wadau mbalimbali ngazi ya mkoa na halmashauri ya wilaya ya Kishapu kupitia idara zake za ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii, sheria, viongozi ngazi ya kata na vijiji, polisi kitengo cha dawati la jinsia na watoto, mahakama na ofisi ya mwendesha mashitaka wa serikali, pamoja na Baraza la Watoto la Wilaya ya Kishapu". Alisema Myola.

Aidha alieleza kuwa mradi huo utatelekezwa kwa kipindi cha miezi sita kwa majaribio katika kata ya Kishapu, Itilima na Bunambiyu na kama mafanikio yataonekana maeneo ya utekelezaji wa mradi yanaweza kuongezwa hivyo kuwataka viongozi wa serikali na jamii kwa ujumla kushirikiana na Agape ili kufanikisha mradi huo.

Naye Msimamizi wa mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto, Felix Ngaiza aliyataja matarajio ya mradi kuwa ni kuongezeka uelewa na ufahamu kuhusu sheria na haki miongoni mwa wanajamii ikiwemo ongezeko la taarifa za kesi za ukatili na uvunjifu wa haki za jinai kwa wanawake na watoto.

Alisema mradi huo pia utachangia katika kufikia lengo la Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) la kufikia 50% ifikapo mwaka 2022.

No comments:

Powered by Blogger.