LIVE STREAM ADS

Header Ads

Watoto wafanyakazu wa nyumbani mkoani Shinyanga wapata ufadhili wa masomo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Shirika la Agape AIDS Control Programme limetoa msaada wa baiskeli kwa watoto wafanyakazi 10 wa nyumbani katika manispaa ya Shinyanga baada ya kuwafadhili kusoma fani mbalimbali katika Chuo Cha Ufundi Stadi (VETA) Mkoa Shinyanga.
Mgeni rasmi wakati wa hafla fupi ya kukabidhi baiskeli hizo, Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga, Boniface Chambi akizungumza kabla ya kukabidhi baiskeli 10 kwa watoto wafanyakazi 10 wa nyumbani waliofadhiliwa na shirika la Agape kusoma fani mbalimbali katika chuo cha VETA Mkoa Shinyanga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agape, John Myola akielezea namna Shirika hilo linavyounga mkono Serikali ya awamu ya tano katika kuwaletea maendeleo wananchi. Kulia ni Msimamizi wa Mradi wa Kumlinda Mtoto Mfanyakazi wa Ndani Dhidi ya Unyonyaji na Unyanyasaji unaotekelezwa na Shirika la Agape, Joyce John, kushoto ni Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga, Boniface Chambi.
Watoto wafanyakazi majumbani wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agape, John Myola.
Baadhi ya waajiri wa watoto wafanyakazi majumbani waliokubali watoto wao wafadhiliwe na Shirika la Agape kupata elimu ya fani mbalimbali katika chuo cha VETA Mkoa Shinyanga.
Msimamizi wa Mradi wa Kumlinda Mtoto Mfanyakazi wa Ndani Dhidi ya Unyonyaji na Unyanyasaji unaotekelezwa na Shirika la Agape, Joyce John akitoa taarifa ya mradi huo huku akitaja changamoto iliyopo kuwa ni ukosefu wa elimu ya haki na wajibu wa watoto wafanyakazi wa nyumbani kwa waajiri na jamii kwa ujumla.
Baiskeli zilizotolewa na shirika la Agape kwa ajili ya watoto wafanyakazi wa nyumbani.
Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga, Boniface Chambi akikabidhi baiskeli kwa mmoja wa watoto wafanyakazi wa nyumbani.
Zoezi la kukabidhi baiskeli likiendelea.
Mmoja wa waliokabidhiwa baiskeli akifurahia tukio hilo.
Mkurugenzi wa Shirika la Agape, John Myola akimpongeza mmoja wa watoto anayekwenda kusoma udereva katika chuo cha VETA.
Mfanyakazi wa nyumbani wa kiume akisindikizwa na mwajiri wake (wa kike ) anayeshikana mkono na Mkurugenzi wa Agape, John Myola.
Watoto wakiwa na baiskeli zao.
Afisa Miradi wa Shirika la Agape, Mustapha Isabuda akiwashauri wazazi na walezi kuwapenda wafanyakazi wa nyumbani na kuepuka kuwanyanyasa.

Na Kadama Malunde - Malunde1 Blog
Shirika la Agape AIDS Control Programme limetoa msaada wa baiskeli kwa watoto wafanyakazi 10 wa nyumbani katika manispaa ya Shinyanga baada ya kuwafadhili kusoma fani mbalimbali katika Chuo Cha Ufundi Stadi (VETA) Mkoa Shinyanga.

Baiskeli hizo 10 zilizotolewa na Shirika la Agape kupitia Mtandao wa Kusaidia Watoto Wafanyakazi wa Nyumbani (Tanzania Child Domestic Workers Coalition – TCDWC) zitasaidia kuwarahisishia usafiri watoto hao kutoka nyumbani kwa waajiri wao hadi chuoni. 

Akizungumza Ijumaa Aprili 5, 2019 wakati wa kukabidhi baiskeli hizo mbele ya Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga Boniface Chambi,Mkurugenzi wa shirika la Agape John Myola alisema msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Kumlinda Mtoto Mfanyakazi wa Ndani Dhidi ya Unyonyaji na Unyanyasaji. 

“Pamoja na kuwapatia baiskeli hizi zenye thamani ya shilingi 110,000/= kila moja,pia tumeshawalipia gharama zote za masomo ya Kozi mwaka mmoja katika fani za udereva,ushonaji,saluni na umeme katika chuo cha VETA kiasi cha shilingi Milioni 1.1 kila mmoja”, alieleza Myola. 

“Agape inapenda kila mtoto hasa watoto wa kike anapata haki ya elimu,tumeona ni vyema kuwapa ujuzi wa kujiendeleza kwenye maisha yao,tunaomba waajiri wawape muda watoto hawa wasome”, aliongeza Myola. 

Kwa upande wake,mgeni rasmi wakati wa hafla fupi ya kukabidhi baiskeli hizo,Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga,Boniface Chambi alilipongeza shirika la Agape kwa kuendelea kuwa wadau muhimu katika kuwaletea maendeleo wananchi kwani wamekuwa wakiunga kwa vitendo jitihada za serikali katika kuwasaidia wananchi. 

“Agape mmekuwa mfano bora,mnajipambanua kwa vitendo kusaidiana na serikali kuwaletea maendeleo wananchi,naomba ‘NGO’s/mashirika mengine pia yafanye kazi za kuonekana badala ya kujinufaisha wenyewe”, alisema Chambi. 

Aidha aliwaasa vijana hao kutunza baiskeli hizo na kuzingatia masomo yao huku akiwataka waajiri kuwapenda wafanyakazi wao wa ndani kwani ni watu muhimu kwa ustawi wa familia hivyo wawape nafasi ya kusoma na kutowanyanyasa. 

Naye Msimamizi wa mradi wa Kumlinda Mtoto Mfanyakazi wa Ndani Dhidi ya Unyonyaji na Unyanyasaji wa shirika la Agape, Joyce John alisema lengo la mradi huo ni kuhakikisha mtoto mfanyakazi nyumbani anawezeshwa kijamii na kiuchumi ili aweze kujikwamua kimaisha. 

“Mradi huu wa miaka mitatu (2016-2019) umejikita katika eneo la kuwapatia mafunzo ya ufundi na idadi ya watoto tuliowafikia hadi sasa ni 75,wengi wao tumewapatia elimu ya ushonaji,ujasiriamali na vitendea kazi ikiwemo cherehani”, alisema John. 

Kwa upande wao, watoto waliopata baiskeli na kufadhiliwa kusoma katika chuo cha Veta walilishukuru shirika la Agape na kuahidi kusoma kwa bidii ili kujikwamua kielimu,kijamii na kiuchumi.

No comments:

Powered by Blogger.