LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la AGAPE laendesha bonanza la michezo kufikisha elimu kwa umma

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na Marco Maduhu, Malunde 1 Blog
Shirika la AGAPE Aids Control Program la mkoani Shinyanga linalojishughulisha na masuala ya jamii, limetoa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa njia ya bonanza la michezo kwenye vitongoji vya Buchamike, Shabuluba, Mwagala na Uswahilini vilivyopo pembezoni mwa Kata ya Usanda Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Bonanza hilo lilifanyika jana kwenye viwanja vya michezo vya kitongoji cha Buchambi Kata ya Usanda likihusisha michezo mbalimbali ikiwemo kukimbiza kuku, mbio za baiskeli pamoja na mpira wa miguu na washindi wamezawadiwa zawadi mbalimbali ikiwamo kupewa kuku pamoja na mbuzi.

Mratibu wa mradi wa afya ya uzazi na jinsia kutoka shirika hilo, Lucy Maganga alisema wameamua kutoa elimu hiyo kwa njia ya michezo ili kufikisha elimu kwa wananchi, kuachana na masuala kupenda kuozesha wanafunzi ndoa za utotoni pamoja na kuwapatia ujauzito na hatimaye kuacha masomo yao. 

Alisema shirika hilo limekuwa likiendesha mradi huo wa afya ya uzazi na ujinsia kwenye kata hiyo tangu mwaka 2017 kwa ufadhili wa shirika la SIDA la nchini Sweden ambao unatarajiwa kuisha mwezi Juni 2019, lakini walikuwa hawafikii wananchi walio pembezoni kutokana na changamoto ya miundo mbinu ya barabara, lakini kwa sasa wameamua kufika hadi maeneo hayo ili elimu hiyo iweze kusambaa maeneo yote. 

"Tumeendesha bonanza hili la michezo kwenye vitongoji ambavyo vipo pembezoni mwaka kata ya Usanda ili kutoa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa rika zote, ambayo itabadilisha mitazamo ya wananchi na kuachana na masuala ya kutongoza wanafunzi pamoja na kuwaozesha ndoa za utotoni ili waweze kutimiza malengo yao" Alisema Maganga na kuongeza;

"Pia tumewataka wananchi kuachana na tabia ya kufanya ngono zembe ambayo yataweza kuwasababishia kupata magonjwa mbalimbali na hatimaye kubakia kujiuguza na kushindwa kufanya shughuli za kimaendeleo na kushindwa kuinuka kiuchumi".

Naye Kaimu Mtendaji wa Kata hiyo ya Usanda, Ester Pembelada alitoa shukrani kwa shirika hilo la AGAPE kwa kutoa elimu hiyo ya afya ya uzazi na jinsia, ambayo imekuwa na msaada mkubwa katika kupunguza changamoto ya mimba na ndoa za utotoni tofauti na hapo awali. 

Baadhi ya wananchi waliohudhuria bonanza hilo akiwemo Edward Ngassa na Lidya Jeremia walisema elimu hiyo itawasaidia kutambua umuhimu wa kusomesha watoto hasa wa kike pamoja na kulinda afya zao. Mratibu wa mradi wa elimu ya afya ya uzazi na jinsia kutoka shirika la Agape, Lucy Maganga akizungumza kwenye bonanza hilo. Kaimu Mtendaji wa kata ya Usanda, Ester Pembelada akizungumza wakati wa bonanza hilo. Baadhi ya wananchi wakifuatilia bonanza hilo.  Baadhi ya wananchi waliohudhuria bonanza hilo. Wananchi wakiendelea kusikiliza elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka Shirika la Agape kwa ufadhili wa shirika la Sida la nchini Sweden. Kwenye mbio za baiskeli, Jumanne Dotto aliibuka mshindi. Mashindano ya baiskeli yakiendelea kwa wanaume ambapo mshindi wa kwanza alipewa zawadi ya mbuzi. Mashindano ya baiskeli yakiendelea kwa wanawake ambapo mshindi ni Lyidia Jeremia na alipewa zawadi ya mbuzi. Mashindano ya kufukuza kuku mshindi ni Milembe Mabula ambapo aliondoka na kuku. Wachezaji wa Kitongoji cha Shabuluba wakiwa kwenye picha ya pamoja kabla ya kuanza mchezo wao wa fainali kwenye bonanza hilo. Timu ya kitongoji cha Buchamike ikiwa kwenye picha ya pamoja. Mchezo wa mpira wa miguu baina ya Buchamike wenye jezi nyeupe pamoja na Shabuluba wenye jezi ya kijani ambapo hadi dakika 90 zinamalizika walitoka sare ya 1-1 na hivyo kuingia kwenye mikwaju ya penati. Mchezaji wa timu ya Shabuluba akipiga penati na kupata goli. Timu ya Buchamike iliibuka na ushindi kwa kupata penati 4-2 dhidi ya Shabuluba.
Kaimu Mtendaji wa Kata ya Usanda, Ester Pembelada (kulia) akikabidhi zawadi ya mbuzi kwa mshindi wa kwanza wa mbio za baiskeli Jumanne Dotto (katikati). Kushoto ni mratibu wa mradi wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka shirika la Agape, Lucy Maganga. Kaimu Mtendaji wa Kata ya Usanda, Ester Pembelada akikabidhi zawadi ya mbuzi kwa washindi wa pili wa timu ya mpira wa miguu ya Shabuluba. Kaimu Mtendaji waKkata ya Usanda, Ester Pembelada akikabidhi zawadi ya mbuzi wawili kwa mshindi wa kwanza wa mpira wa miguu kutoka timu ya Buchamike. Kushoto ni mratibu wa mradi wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka shirika la Agape, Lucy Maganga.

No comments:

Powered by Blogger.