LIVE STREAM ADS

Header Ads

MISA Tanzania yasisitiza umoja ili kupambana na ukiukwaji wa uhuru wa habari

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) tawi la Tanzania imesisitiza umoja na mshikamano baina ya wadau na taasisi za habari kote duniani ili kupambana na viashiria vinavyokwamisha uhuru wa habari.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Sengiyumva Gasirigwa (pichani) ameyasema hayo hii leo Mei 03, 2019 kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani 2019 yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma. 

“Maadhimisho haya yatupe changamoto ya kutafakari uhuru wa vyombo vya habari duniani na kuwakumbuka wanahabari waliokumbana na kadhia mbalimbali ikiwemo kupoteza maisha kutokana na kazi zao ambapo ili kuyashinda haya tunahitaji umoja madhubuti”, amesisita Gasirigwa.

Wakati Gasirigwa anasisitiza hayo, shirika la umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), linaripoti kwamba tangu mwaka 1994 hadi mwaka 2018 waandishi 1307 duniani kote wamepoteza maisha wakiwa kazini huku mwaka jana pekee waandishi 99 wakiuawa hivyo viashiriwa vinavyohatarisha uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari havipaswi kupuuziwa. 

Hivyo Mei 3 kila mwaka iliteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa siku maalumu ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ikiwa ni tarehe ambayo Jubilee ya Azimio la Windhoek lililoketi mwaka 1991 nchini Ethiopia liliazimia siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Itakumbukwa kwamba Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulioketi mwaka 1993 uliyapitia mapendekezo kadhaa ya shirika la Unesco lililoketi mwaka 1991 nchini Ethiopia ambapo pendekezo mojawapo lilikuwa kuitambua siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani. 

Aidha pamoja na mambo mengine, siku hii imelenga kuzikumbusha Serikali kote duniani kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari kwa kuwalinda dhidi ya vitisho, manyanyaso, kuuawa, kufungwa, kutozwa faini huku umma ukijulishwa juu ya ukiukwaji wa haki hizo kote duniani. 

Nchini Tanzania, taasisi mbalimbali zimeshiriki kufanikisha maadhimisho hayo ikiwemo MISA Tanzania, Ubalozi wa Marekani, Internews, FES, IMS, Umoja wa Mataifa, UTPC, TMF, TEF, UK Aid, TAMWA, MCT, Unesco na Serikali ya Tanzania huku kauli mbiu ikiwa ni “Vyombo vya Habari kwa Demokrasia, Tasnia ya Habari na Uchaguzi nyakati za upotoshwaji wa taarifa”.

Tazama picha kutoka jijini Dodoma yanapofanyika maadhimisho hayo kitaifa

No comments:

Powered by Blogger.