LIVE STREAM ADS

Header Ads

Taasisi ya MISA Tanzania yatoa mafunzo kwa wanahabari kuhusu habari za jinsia

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) tawi la Tanzania kwa kushirikiana na ile ya VIKES ya nchini Finland, imeandaa mafunzo ya kwa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa ili kuwajengea uwezo wa kuripoti habari za kijinsia kwa weledi.

Mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika jijini Mwanza kuanzia leo jumamosi Mei 18, 2019 yakiwashirikisha waandishi wa habari 25 kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Shinyanga pamoja na Simiyu.

Mkurugenzi wa MISA Tanzania, Sengiyumva Gasirigwa amesema mafunzo hayo pia yamelenga kuwajengea uwezo waandishi wa habati katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ili kuibua na kuripoti habari mbalimbali za kijinsia hususani zinazowagusa wanawake kwani wamekuwa hawapewi kipaumbele na vyombo vya habari.

"Tunahitaji kubadili fikra katika kuripoti habari za kijinsia, bado wanaume wanapewa kipaumbele huku wanawake wakisahaulika hivyo mafunzo haya yatusaidie kutoka tuliko na kuanza kuibua mambo mazuri yanayofanywa na wanawake na kuyaripoti kupitia vyombo vyetu vya habari", amesisitiza Gasirigwa.

Akiwasilisha mada ya jinsia kwenye mafunzo hayo, Alex Mchomvu kutoka Chuo Kikuu cha SAUT Mwanza amesema baadhi ya mila na desturi zimekuwa zikiathiri masuala mbalimbali ya usawa wa kijinsia hivyo waandishi wa habari wanapaswa kutumia vyombo vya habari kubadili hali hiyo ili kuleta usawa kwenye masuala ya kijinsia.

Naye Kenneth Simbaya, Mwenyekiti Mtandao wa Waandishi wa Habari za Afya Tanzania (Africa Media Network on Health Accountability Tanzania Chapter), akiwasilisha mada kuhusu misingi ya uandishi wa habari amehimiza waandishi wa habari kuiishi misingi hiyo ikiwemo ukweli na usahihi bila kupendelea kwani wamepewa dhamana kubwa katika jamii.

“Kuna wasiwasi mkubwa kwa sasa juu ya utendaji wa wanahabari ambapo ukweli ni kwamba jamii haituamini tena. Lakini imani au kuaminika ni jambo la muhimu katika kazi yetu kama wanahabari” amesema Simbaya na kuongeza;

“Ili kurudisha imani hiyo ni lazima waandishi wa habari na vyombo vya habari kuiishi misingi au miiko ya wanahabari ambayo ni ukweli na usahihi, uhuru (kutokuwa tegemezi), kuzingatia usawa (fairness and impartiality), utu (humanity) na uwajibikaji (Accountability)” amesisitiza Simbaya.

Washiriki wameishukru taasisi ya MISA Tanzania kwa kuandaa mafunzo hayo wakisema yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi ikiwemo kuandaa habari na makala mbalimbali kuhusu usawa wa kijinsia kwa kutoa nafasi sawa baina ya wanawake na wanaume tofauti na ilivyo sasa ambapo asilimia kubwa ya vyanzo vyao ni wanaume wakati kuna wanawake wengi wanafanya mambo makubwa lakini habari zao hazipati nafasi.
Mkurugenzi wa MISA Tanzania, Sengiyumva Gasirigwa akitoa ufafanuzi kwa washiriki kuhusiana na mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu kuripoti habari za kijinsia kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wakimsikiliza Mkurugenzi wa MISA Tanzania, Sengiyumva Gasirigwa.
Mmoja wa wakufunzi, Alex Mchomvu kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Kampasi Kuu ya Mwanza akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Mmoja wa wakufunzi, Kenneth Simbaya ambaye pia ni Mwenyekiti Mtandao wa Waandishi wa Habari za Afya Tanzania (Africa Media Network on Health Accountability Tanzania Chapter) akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Mmoja wa washiriki, Erica Elias kutoka mkoani Shinyanga akichangia mada kwenye mafunzo hayo.
Wakufunzi wa mafunzo hayo, Alex Mchomvu kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Kampasi Kuu ya Mwanza (kushoto) pamoja na Kenneth Simbaya (kulia) ambaye pia ni Mwenyekiti Mtandao wa Waandishi wa Habari za Afya Tanzania (Africa Media Network on Health Accountability Tanzania Chapter).
Mkurugenzi wa MISA Tanzania, Sengiyumva Gasirigwa (katikati), akiteta jambo na wakufunzi wa mafunzo hayo ambao ni Alex Mchomvu (kushoto) pamoja na Kenneth Simbaya (kulia).
Washiriki wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kuripoti habari za kijinsia.
Mshiriki Erica Elias akiwasilisha mada kwa niaba ya wanakundi wenzake.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo akiwasilisha mada kwa niaba ya washiriki wenzake.
Mshiriki Beatrice Rabach kutoka jijini Mwanza pamoja na wenzake wakiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.

No comments:

Powered by Blogger.