LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la AGPAHI lasaidia wananchi mkoani Simiyu kupima afya bure

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Shirika la AGPAHI (Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative) linalojishughulisha na mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi nchini Tanzania, limetoa huduma ya upimaji afya bure kwa wananchi mkoani Simiyu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani 2019 ambayo kilele chake ni Mei 05 kila mwaka.

Huduma hiyo imetolewa katika uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi yalikofanyika maadhimisho hayo ambapo wananchi hususani akina mama walipata fursa ya kufanya uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa Kizazi pamoja na VVU kuanzia Mei 02, 2019.

Akitoa takwimu za awali jana kabla hatujaenda mitamboni, Mratibu wa Shirika la AGPAHI mkoani Simiyu, Dafrosa Shiluka alisema zaidi ya akina mama 200 walifanyiwa uchunguzi na kati hao, mmoja aligundulika kuwa na dalili za awali za Saratani ya Mlango wa Kizazi na kuanzishiwa huduma ya mgandisho katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Simiyu, Somanda huku wengine wawili wakipewa rufaa.

“Lakini pia akina mama wawili walikutwa na Saratani ya Mlango wa Kizazi ambapo tuliwapa rufaa ya kwenda Bugando (Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa) kwa ajili ya matibabu zaidi” alieleza Shiluka.

Shiluka pia aliongeza kwamba akina mama 166 walikubali kupima maambukizi ya VVU ambapo kati yao, mmoja alikundulika kuwa na maambukizi ya VVU na kuanzishiwa dawa kupitia Kituo cha Afya Muungano.

“AGPAHI tunatoa huduma za tiba na matunzo kwa wanaoishi na maambukizi ya VVU katika Wilaya zote za Mkoa Simiyu ambapo tuna jumla ya Vituo 73 ambavyo tunavihudumia kwa ajili ya huduma hiyo na Vituo vinane kati ya 73 vinatoa huduma ya uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa Kizazi” alisema Shiluka.

Shiluka alitoa rai kwa wananchi hususani akina mama kuwa na desturi ya kujitokeza kupima saratani ya mlango wa kizazi kwenye Vituo vya Afya na Hospitali zinazotoa huduma hiyo tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi hujitokeza tu kwenye makongamano mbalimbali mkoani Simiyu.

Baadhi ya akina mama waliojitokeza kufanya uchunguzi kwenye maadhimisho hayo walitoa shukrani kwa Shirika la AGPAHI kwa kutoa huduma hiyo na kuahidi kuitumia vyema elimu waliyoipata ikiwemo kuhamasisha wenzao kwenda katika Vituo vya Afya na Hospitali kufanya uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa Kizazi na Matiti.

“Tumefundishwa jinsi ya kuambukizwa na jinsi ya kujikinga, ukikutwa hauna Saratani ya Mlango wa Kizazi hautakiwi uwe na wanaume wengi, tujikinge, tuwe watulivu na tupime mara kwa mara” alisema Pendo Mboje.

Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, Dkt. Faustine Ndungulile ambaye ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto aliwahamasisha wananchi kupima afya zao ikiwemo VVU na Saratani ya Mlango wa Kizazi huku akiongeza kwamba Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya nchini ili kuwaondolea wananchi adha ya kupata matibabu.
Mratibu wa Shirika la AGPAHI mkoani Simiyu, Dafrosa Shiluka akizungumza na BMG kwenye maadhimisho hayo.
Pendo Mboje ambaye ni Mkazi wa Bariadi akizungumza na BMG kuhusu huduma ya upimaji iliyotolewa na Shirika la AGPAHI.
Mkuu wa Wilaya Busega, Festo Kiswaga akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani 2019 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Simiyu, Antony Mtaka.
Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile akizungumza kwenye maadhimisho hayo kwa niaba ya Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan.
Washiriki wa Siku ya Wakunga Duniani 2019 yaliyofanyika kitaifa Bariaadi mkoani Simiyu wakiwasili uwanjani.
Viongozi mbalimbali kwenye maadhimisho hayo akiwemo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile (wa tatu kushoto), Mkuu wa Wilaya Busega Festo Kiswaga (wa pili kulia),  Rais wa TAMA Feddy Mwanza (wa tatu kulia), Makamu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA) nchini Tanzania, Dkt. Hashina Begum (wa pili kulia) pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa Simiyu (wa kwanza kushoto).
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile akisikiliza ufafanuzi alipotembelea banda la Shirika la AGPAHI.
Mratibu wa Shirika la AGPAHI mkoani Simiyu, Dafrosa Shiluka (kushoto) akitoa ufafanuzi wa huduma zinazotolewa na Shirika hilo kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile  (kulia).
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile akipokea kipeperusha chenye elimu kuhusu Saratani ya Mlango wa Kizazi alipotembelea banda la Shirika la AGPAHI.
Sehemu ya akina mama waliojitokeza kupata huduma ya uchunguzi kwenye banda la Shirika la AGPAHI.
Mratibu wa Shirika la AGPAHI mkoani Simiyu, Dafrosa Shiluka akitoa ufafanuzi kwa mmoja wa wananchi waliofika kwenye banda la Shirika hilo.
Sehemu ya akina mama waliojitokeza kupata huduma ya uchunguzi kwenye banda la Shirika la AGPAHI.
Baadhi ya Wakunga waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani 2019 kitaifa mjini Bariadi.
Tazama BMG Online TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.