LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wakunga Tanzania waomba Serikali kuboresha mazingira yao ya kazi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), Feddy Mwanga amesema mchango wa wakunga unafikia asilimia 87 katika kuokoa maisha ya mama na mtoto kabla na baada ya kujifungua.

Ameomba Serikali iendelee kutambua mchango wa wakunga ikiwemo upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na nyumba za wakunga kwenye Vituo vya Afya na Hospitali kama ilivyo kwa Waganga kwani nao wanafanya kazi masaa 24 hususani kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Mwanga amesema katika kampeni ya kitaifa ya Jiongeze, Tuwavushe Salama inayolenga kupunguza vifo vya uzazi, Wakunga wana asilimia zaidi ya 50 katika kuifanikisha.

Hata hivyo amewahimiza Wakunga Tanzania kuendelea kutoa huduma kwa weledi na staha kwani hakuna mtaala unaofundisha matusi hivyo si vyema baadhi yao kulalamikiwa kwa kutoa lugha chafu kwa wateja hususani akina mama wakati wa kujifungua.

Hii ni sehemu ya hotuba ya Rais Mwanga aliyoitoa kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani yanayofanyika kitaifa Bariadi mkoani Simiyu yakiwa na kauli mbiu "Wakunga ni Watetezi wa Haki za Wanawake".

Naibu Waziri wa Afya, Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndungulile ametumia maadhimisho hayo kupongeza kazi kubwa inayofanywa na Wakunga nchini na kuongeza kwamba Serikali itaendelea kuboresha mazingira yao ya kazi ikiwemo vitendea kazi na nyumba hususani maeneo ya vijijini.

Naye Makamu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA) nchini Tanzania, Dkt. Hashina Begum amesema kazi nzuri inayofanywa na Wakunga imesaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto kabla, wakati na baada ya kujifungua hivyo shirika hilo litaendelea kutoa ushirikiano wake katika kuboresha huduma zao.

Huduma mbalimbali zinatolewa bure kwa wananchi kwenye maadhimisho hayo tangu Mei 02, 2019 ikiwemo upimaji wa Saratani ya Mlango wa Kizazi unaosimamiwa na shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) ambapo wananchi hususani akina mama wamefurahia huduma hiyo.

Chama cha TAMA kimeratibu maadhimisho hayo ikiwa ni mwaka wa 27 mwaka huu tangu kianzishwe mwaka 1992 ambapo wadau mbalimbali ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFP), AGPAHI, Jhipiego, Amref, Marie Stopes, USAID Boresha Afya, IntraHealth, Tanzania Health Promotion, Cuuam, TAMA PPIUD, TCDC, Cuso International, NMB pamoja Jambo Group wakisaidia kufanikiwa kwake.
Wakunga wakiigiza namna ya kumsaidia mama mjamzito wakati wa kujifungua ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Rais wa TAMA Taifa, Feddy Mwanza akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani 2019 yaliyofanyika Bariadi mkoani Simiyu.
Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndungulile akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Makamu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA) nchini Tanzania, Dkt. Hashina Begum akitoa salamu za shirika hilo kwenye maadhimisho hayo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Faustine Ndungulile (kulia), akipata maelezo kuhusu huduma zinazotolewa na shirika la AGPAHI alipotembelea banda la shirika hilo kwenye maadhimisho hayo.

No comments:

Powered by Blogger.