Header Ads

Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani 2019 kufanyika mkoani Simiyu kitaifa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mkuu wa Mkoa Simiyu, Anthony Mtaka (katikati) akizungumzia Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo kitaifa yanafanyika leo Mei 05, 2019 katika uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani humo.
Makamu Mwakilishi Mkaazi wa shirika la UNFPA nchini Tanzania, Dkt.Hashina Begum (wa pili kushoto) akizungumzia maadhimisho hayo.
Rais Chama Cha Wakunga Tanzania (TAMA), Feddy Mwanga (katikati) akitoa taarifa kuhusu maadhimisho hayo kupitia mkutano uliowajumuisha waandishi wa habari (hawako pichani).
Baadhi ya waandishi wa habari wa mkoani Simiyu wakinasa taarifa kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani 2019 yanayofanyika mjini Bariadi leo.

Na Stella Kalinga, Simiyu
Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani kitaifa mwaka 2huu 019 yanafanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akimwakilisha Makamu wa Rais wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza jana na waandishi wa habari ofisini, Mkuu wa Mkoa Simiyu, Anthony Mtaka aliwakaribisha wakunga wote hapa nchini na kuwahakikishia kuwa Mkoa umefanya maandalizi ya kutosha ili maadhimisho hayo yaweze kufana.

"Nitumie nafasi hii kuwaalika Wakunga wote Tanzania ambao wameanza safari kuja kwenye shughuli yao kitaifa ndani ya Mkoa wetu, niwahakikishie kuwa tumefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha shughuli yao inaenda vizuri" alisema Mtaka.

Katika hatua nyingine Mtaka alishukru shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu Duniani (UNFPA) kwa kuwezesha maadhimisho hayo kitaifa kufanyika mkoani Simiyu pamoja na mchango mkubwa wa shirika hilo na wadau wengine katika sekta ya afya mkoani humo..

Naye Makamu Mwakilishi Mkaazi wa shirika la UNFPA hapa nchini, Dkt. Hashina Begum alisema kauli mbiu ya Siku ya Wakunga Duniani 2019 ni "Wakunga ni Watetezi wa Haki za Wanawake" ikilenga kukumbusha umuhimu wa wakunga katika kuwatetea akina mama wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua.

Aliongeza kuwa shirika la UNFPA litaendelea kushirikiana na Serikali katika ukarabati wa vituo 38 vya afya, wodi za wazazi, vyumba vya upasuaji, ununuzi wa vifaa na mashine za kumwezesha Mkunga kutoa huduma ya mama na mtoto kwa urahisi na kuwajengea uwezo wakunga 90 kutoka vituo vilivyokarabatiwa kutoa huduma za dharura kwa mama na mtoto.

Naye Rais Chama Cha Wakunga Tanzania (TAMA), Feddy Mwanga alisema chama hicho kinafanya kazi na Mkoa wa Simiyu tangu mwaka 2016kwa kuwaelimisha Wakunga ili kutoa huduma za dharura kwa mama na mtoto hususani katika vituo vya pembezoni huku akilishukru shirika la UNFPA kwa mchango wake wa kifedha na utaalamu kuwezesha mafunzo hayo.

Aliongeza kwamba Dira ya TAMA ni kuona kila mama mjamzito na watoto wachanga wanahudumiwa na Wakunga wataalam na wanapata huduma bora huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye Maadhimisho hayo ili waweze kupata huduma za upimaji bila malipo.

No comments:

Powered by Blogger.