LIVE STREAM ADS

Header Ads

Dkt. Kijazi ashinda kwa kishindo nafasi ya Makamu wa tatu wa Rais WMO

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Na Monica Mutoni, Geneva
Kwa mara nyingine Tanzania imeingia katika historia ya kimataifa baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye pia ni Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi kuibuka mshindi wa nafasi ya Makamu wa tatu wa Rais wa shirika la WMO.

Dkt. Kijazi anachukua nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2019-2022 akiwa mwanamke wa kwanza na Mjumbe wa kwanza kutoka nchi zinazoendelea kushika nafasi hiyo ambapo atakuwa na majukumu makubwa ya kumsaidia Rais wa WMO kuongoza Shirika hilo katika kutekeleza majukumu yake yenye tija kwa wanachama wake ikiwemo Tanzania.

Akizungumzia ushindi wake mbele ya wapiga kura wa mkutano wa 18 wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) pamoja na wajumbe waalikwa, Dkt. Kijazi alitoa shukrani zake za dhati kwa wote waliomwamini na kumuunga mkono hadi kushinda nafasi hiyo na kuahidi kuitumikia kwa weledi wa hali ya juu ili kufikia malengo ya Shirika hilo.

"Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wote waliokuwa pamoja na mimi kwa kuniunga mkono na kunichagua kwa kura zote, naahidi kuitumikia nafasi hii kwa weledi mkubwa na kuhakikisha WMO inafikia malengo yake" aliisema Dkt. Kijazi.

Akizungumzia ushundi huo, Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Atashasta Nditiye alisema ni heshima kubwa sana kwa Tanzania na kwamba Wizara hiyo inampongeza Dkt. Kijazi huku ikiamini ataiwakilisha nchi vizuri. 

Aidha alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa ushirikiano aliouonesha kwa kukubali Tanzania kuwakilishwa na Dkt. Kijazi ambapo kwa jitihada zake katika kuboresha sekta ya hali ya hewa zimeendelea kuiletea sifa nchi kwa ujumla.

Kwa upande wa Kaimu Balozi, Ubalozi wa Kuduma Umoja wa Mataifa Geneva nchini Uswizi, Ndugu Robert Kahendaguza alisema ushindi wa Dkt. Kijazi ni kielelezo cha umadhubuti wa diplomasia ya Tanzania na sifa zake binafsi ikiwemo uzoefu wa muda mrefu pamoja na elimu ya ngazi ya juu katika nyanja ya sayansi ya hali ya hewa.

Pia aliongeza kuwa sababu za sifa hizo ziliupunguzia ubalozi kazi ya kumnadi na hata kuwa rahisi kuishawishi nchi ya Sudan kuondoa mgombea wao na hivyo kumfanya Dkt. Kijazi kuwa mgombea pekee katika nafasi yake.

Uchaguzi wa viongozi wa WMO hufanyika kila baada ya miaka minne kwa kuchagua viongozi mbali mbali wakiwemo Katibu Mkuu, Rais, Makamu wa Rais wa kwanza, Makamu wa Rais wa pili na Makamu wa Rais wa tatu ambapo kwa mwaka huu 2019 umefanyika katika mkutano wa 18 wa shirika hilo baada ya muda wa viongozi waliokuwepo kufikia ukomo.

Uchaguzi huo ulifanyika Juni 13, 2019 kwa haki na kwa amani na kuwapata viongozi wapya ambao ni Profesa Petteri Taalas kutoka Finland (Katibu Mkuu), Profesa Dkt. Gerhard Adrian kutoka Ujerumani (Rais), Profesa Celeste Saulo kutoka Argentina (Makamu wa kwanza wa Rais), Dkt. Albert Martis kutoka Curacao (Makamu wa pili wa Rais) pamoja na Dkt. Agnes Kijazi kutoka Tanzania (Makamu wa tatu wa Rais).

No comments:

Powered by Blogger.