LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mbunge Viti Maalum Mkoa Shinyanga asaidia uboreshaji huduma za afya

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa Shinyanga, Azza Hilal Hamad (CCM) amechangia shilingi 5,895,000/= kwa ajili ya upauaji wa jengo la wodi ya akina mama katika Zahanati ya Kijiji cha Zunzuli, Kata ya Mwenge Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara ulichohudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko uliofanyika jana katika Kijiji cha Zunzuli, mbunge huyo alisema fedha hizo zitatumika kununua mbao na mabati kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya akina mama.

"Baada ya kuona Zahanati hii ya Zunzuli haina wodi ya akina mama, nilichokifanya ni kutafuta fedha kwa ajili ya upauaji, namshukuru Mungu wadau wangu wamenishika mkono, nimepata kiasi cha shilingi milioni 5.8 kwa ajili ya kununua mbao na mabati ili wodi hii ya wazazi ambayo wananchi wameijenga hadi kwenye renta ili iweze kupauliwa" alisema Azza.

"Zahanati hii ya Zunzuli iliyojengwa mwaka 1994 ina chumba kidogo tu chenye vitanda viwili, akina mama wanapokuwa wengi huduma inakuwa tatizo, takwimu zinaonesha Zahanati hii inapokea akina mama wanaojifungua kati ya 20 hadi 25 kwa mwezi ndiyo maana nikaona umuhimu wa kuwatafutia fedha za upauaji ili akina mama waweze kupata huduma wanayostahili" aaliongeza Azza.

Alisema jukumu lake kubwa kama Mbunge wa Viti Maalum ambaye pia ni mwanamke ni kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa na hiyo ni kuunga mkono kwa vitendo jitihada zinazofanywa na Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli katika kuboresha sekta ya afya.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Shinyanga, Jasinta Mboneko aliwataka wananchi kutumia fedha zilizotolewa na mbunge huyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwakumbusha kuwa mstari wa mbele kuchangia shughuli za maendeleo badala ya kusubiri serikali pekee iwaletee maendeleo.

Mboneko pia aliwahamasisha wanawake kuhudhuria kliniki na kujifungulia kwenye Vituo vya Afya huku akiwasisitiza akina baba kutunza na kukaa vizuri na wake zao badala ya kuwanyanyasa na kupeleka watoto shule badala ya kuwaozesha. 
Diwani wa Kata ya Mwenge, Edward Maganga (wa pili kulia) akimwongoza Mbunge wa Viti Maalum Mkoa Shinyanga, Azza Hilal Hamad (wa pili kushoto) na Mkuu wa Wilaya Shinyanga, Jasinta Mboneko (katikati) walipowasili katika Zahanati ya Zunzuli.
Muonekano wa jengo la wodi ya akina mama katika Zahanati ya Zunzuli iliyopo Kata ya Mwenge.
Mganga Mfawidhi Zahanati ya Zunzuli, Dkt. Manumi Julius akionyesha jengo la Zahanati ya Zunzuli.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa Shinyanga, Azza Hilal Hamad (CCM) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Zunzuli.
Mkuu wa Wilaya Shinyanga, Jasinta Mboneko akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Shinyanga, Hoja Mahiba akizungumza kwenye mkutano huo.

No comments:

Powered by Blogger.