LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wadau washerehekea Sikukuu ya Eid El Fitr na watoto wenye mahitaji maalum

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na Kadama Malunde, Malunde 1 Blog
Shirika lisilo la kiserikali la Investing in Childrean and Societies (ICS Africa) kwa kushirikiana na watanzania waishio Denmark, shirika la CIS na familia ya Robert Mugeta iliyopo Marekani wamesherekea sikukuu ya Eid El-Fitr pamoja na watoto wenye mahitaji maalumu (wenye ualbino, viziwi na wasioona) waliopo katika bweni la Shule ya Msingi Buhangija "Kituo cha Buhangija" Mjini Shinyanga. 

Wadau hao wa watoto wameungana na watoto hao jana Juni 5, 2019 kusherehekea sikukuu hiyo kwa kucheza, kunywa, kula pamoja na kuwapa zawadi mbalimbali ikiwemo sabuni, pipi na biskuti.

Akizungumza wakati wa sherehe hizo, Meneja wa Shirika la ICS nchini Tanzania linalohusika na masuala mbalimbali ikiwemo malezi na makuzi bora ya watoto, ulinzi na usalama kwa watoto, Kudely Sokoine Joram alisema wanapenda watoto hivyo furaha yao ni kuona watoto hao wanafurahi kama watoto wengine katika jamii. 

"Tumefanikisha jambo hili kwa kushirikiana na watanzania wenzetu waishio Denmark, shirika la CIS la Denmark na familia ya Robert Mugeta iliyopo Marekani. Tumekuja hapa kusherehekea na watoto sikukuu ya Eid El Fitr lengo ni kuwafanya watoto hawa wajisikie wanathaminiwa, wanapendwa na tunawajali waone kuwa wao ni sehemu ya jamii" alisema Sokoine. 

"Watoto hawa wengi wakiwa ni wenye ualbino wanaishi pamoja hapa Buhangija, tumeona ni vyema kusherehekea nao pamoja tofauti na watoto waliopo majumbani ili kuwapa furaha. Tunashukru serikali na uongozi wa shule kwa kuturuhusu kujumuika nao. Kwa kweli watoto wamefurahia sana" alisema Sokoine. 

Sokoine aliongeza wataendelea kushirikiana na wadau wote wakiwemo watanzania hawa waliopo Denmark, Marekani pamoja serikali kuhakikisha wanapata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili shule ya Buhangija ikiwemo kuhakikisha watoto hao wanakua salama na kupata haki zao za msingi ikiwemo mazingira salama. 

"Sisi ICS Africa kwa kushirikiana na marafiki zetu pamoja na wadau wengine tutaendelea kushirikiana na serikali kutatua changamoto zilizopo hapa, tukio la leo ni hatua za mwanzo za kutengeneza mahusiano lakini Mwenyezi Mungu akitujalia tuna kazi kubwa ya kufanya hapa shuleni siku zijazo" alisema. 

Aidha aliwataka watoto hao kuwa watiifu, kufuata maelekezo wanayopewa na walimu na kusoma kwa bidii, kushirikiana na kuwapenda wenzao ili waweze kutimiza ndoto zao. Kwa upande wao, watoto hao walieleza kufurahia ujio wa wadau hao huku wakizitaja baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni ukosefu wa fensi na taa kwenye mabweni mapya yaliyojengwa hivyo kuomba wadau kujitokeza kuwasaidia.
Meneja wa shirika la ICS Africa Tanzania, Kudely Sokoine Joram akizungumza na watoto wenye ualbino,wasioona na wenye uziwi katika bweni la Shule ya Msingi Buhangija.
Meneja wa shirika la ICS Africa Tanzania, Kudely Sokoine Joram akizungumza na watoto hao.
Meneja wa Shirika la ICS Africa Tanzania, Kudely Sokoine Joram na watoto wakizungumza mubashara kwa njia ya simu 'Video Call' na watanzania waishio Denmark .
Kulia ni Meneja wa shirika la ICS Africa Tanzania, Kudely Sokoine Joram akikabidhi zawadi ya sabuni za kufulia maboksi nane kwa ajili ya watoto hao.
Watoto wakishindana kucheza muziki.
Meneja wa shirika la ICS nchini Tanzania, Kudely Sokoine Joram akicheza wimbo wa Diamond Platnmuz 'Tetema' na Watoto.
Meneja wa shirika la ICS Tanzania, Kudely Sokoine Joram akitoa zawadi kwa watoto.
Afisa Huduma kwa jamii kutoka idara ya huduma za uangalizi, Wizara ya Mambo ya Ndani, Monica Dawa akigawa juisi kwa watoto.
Zoezi la kugawa zawadi likiendelea.
Watoto wakilishukru shirika la ICS na watanzania waishio Denmark.
Mshereheshaji wakati wa sherehe hizo, Mwalimu Jackson Leonard akitoa neno la shukrani.
Mwalimu mlezi wa watoto hao, Flora Gelard akieleza changamoto walizonazo.
Misosi "time".
Afisa huduma kwa jamii kutoka Idara ya huduma za uangalizi, Wizara ya Mambo ya Ndani, Monica Dawa akiwahudumia watoto hao.
Huku Meneja wa shirika la ICS Africa Tanzania, Kudely Sokoine Joram akiwahudumia watoto hao.
Wadau wakiwa katika picha ya pamoja na watoto wenye mahitaji maalumu Buhangija.
Kikosi kilichofanikisha maandalizi ya sherehe za sikukuu ya Eid El Fitr kwa watoto wenye ualbino, wasioona na wasiosikia katika bweni la Buhangija mjini Shinyanga.

No comments:

Powered by Blogger.