LIVE STREAM ADS

Header Ads

Hili hapa ombi la wanawake wajasiriamali Tanzania kwa Serikali

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Judith Ferdinand, BMG
Wanawake wajasiriamali mkoani Mwanza wameiomba Serikali kupunguza masharti ya upataji nembo ya ubora wa bidhaa kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kurahisisha mazingira ya ufanyaji biashara zao.

Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) Mkoa wa Mwanza, Mariam Munanka kwenye mkutano wanachama wa chemba hiyo pamoja na wadau mbalimbali uliofanyika jijini Mwanza.

"Ili kupata nembo ya ubora kutoka TBS unatakiwa uwe umekidhi vigezo husika ikiwemo jengo lenye kiwango ambalo thamani yake si chini ya milioni 10, ukiangalia mjasiriamali ana mtaji wa milioni moja masharti ambayo si rahisi kutimiza na kufanikiwa kuipata hivyo ombi letu kwa Serikali ni kupunguza masharti magumu ili kumuwezesha mjasiriamali kupata fursa za masoko ndani na nje ya nchi" alisema Munanka.

Afisa Maendeleo na Biashara wa mradi wa kuwasaidi na kuwaendeleza wajasiriamali Tanzania (TLED) kutoka Shirika la Volunteers Services Oversees (VSO), Henry Shimba alisema kwa kushirikiana na SIDO na TWCC wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wajasiriamali kuhusu usimamizi wa fedha, biashara, usalama kazini na utafutaji wa masoko.

"Tumekuwa tunawajengea uwezo wanawake wafanyabiashara wa masoko kwa kuwapatia mafunzo ambayo yanaendana na Sera ya taifa ya uchumi wa viwanda pamoja na kuwaunganisha na taasisi zinazohusika na utoaji wa vibali kama TBS" alisema Shimba.

Kwa upande wake Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mwanza (Menejimenti ya Madeni), Sylver Rutangwelera aliwahimiza wajasiriamali kutunza kumbukumbu za biashara zao kwani mali bila daftari hupotea bila kujua huku akiwataka wenye mtaji kuanzia milioni 14 kutumia mashine za kutolea stakabadhi za kielektroni (EFD's).

No comments:

Powered by Blogger.