Shirika la AGPAHI lilivyoshiriki maadhimisho ya Ukimwi kitaifa jijini Mwanza
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na George Binagi-GB Pazz, BMGShirika la AGPAHI linalojihusisha na mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi limeshiriki maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza kuanzia Novemba 25, 2019 hadi Disemba 01, 2019 kwa kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya afya kwa wananchi.
Katika
maadhimisho hayo, Shirika la AGPAHI lilitoa elimu kuhusu masuala mbalimbali
ikiwemo maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi, huduma ya tiba na matunzo
kwa vijana, matumizi sahihi ya dawa pamoja na kufanya bure uchunguzi wa
saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake huku waliopatikana na dalili za awali
wakiunganishwa katika huduma za matibabu.
Aidha
shirika la AGPAHI lilitumia maadhimisho hayo kuhamasisha wananchi kuwa wawazi
na kujua afya zao kwa kujitokeza kupima maambukizi ya Vizuri vya Ukimwi kwa
hiari huku wale wanaopatikana na maambukizi hayo wakishauriwa kutambua umuhimu
kuzingatia matumizi sahihi ya dawa.
Naye mmoja
wa vijana jijini Mwanza ambaye anaishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, Christina
Peter alilishukuru Shirika la AGPAHI kwa kuwapa elimu kuhusu masuala mbalimbali
ikiwemo elimu ya uzazi wa mpango, jinsi ya kuwa kwenye mahusiano salama na
kuzaa watoto wasio na maambukizi pamoja na ujuzi wa ujasiriamali unaowasaidia
kujikimu kimaisha.
“Napenda
kuwashauri vijana wenzangu kuwa wawazi kwa kupima afya ili wajue hali zao kwani
kuishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi haimaanishi kwamba maisha yako yameharibika
bali ukiisha ikubali hali yako unaweza kutimiza malengo yako makubwa”
alisisitiza Christina Peter ambaye alizaliwa na VVU miaka 22 iliyopita na
kuongeza kwamba suala la unyanyapaa halipaswi kupewa nafasi na mtu yeyote.
Katika hatua
nyingine Shirika la AGPAHI pia lilitumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi
hususani vijana ili kujiepusha na matumizi ya madawa ya kulevya ambayo yamekuwa
yakichochea baadhi yao kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Wakitoa rai
kwa wenzao kujiepusha na matumizi ya madawa ya kulevya, Boniphace Wanjara
pamoja na Shoma Masanja ambao walikuwa wahanga madawa hayo walisema Shirika la
AGPAHI limewasaidia kupata matibabu kupitia huduma ya medhadoni katika Hospitali
ya Sekou Toure na sasa wamekuwa mabalozi wa kutoa elimu kwa vijana wenzao kujiepesha
na matumizi ya madawa ya kulevya kwani yana madhara makubwa.
“Kwa kiwango
kikubwa Shirika la AGPAHI limekuwa likitudhamini kwa hali na mali ili kumudu
gharama za uendeshaji wa kitengo pamoja na kuwakwamua vijana wengi kutoka
kwenye dimbwi hili la madawa ya kulevya” alibainisha Euphrasia Valerian ambaye
ni Muuguzi Hospitali ya Sekou Toure.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama (kushoto) akipata ufafanuzi wa shughuli zinazofanywa na Shirika la AGPAHI alipotembelea banda la Shirika hilo kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kitaifa katika viunga vya Rock City Mall jijini Mwanza.
Tazama BMG TV ONLINE hapa chini
No comments: