Wakazi wa Shinyanga watakiwa kutunza miradi ya maji
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji katika eneo la Uzogole, Lubaga pamoja na Masengwa, miradi ambayo itawaondelea changamoto wananchi ya ukosefu wa maji safi na salama.
Mboneko amefanya ziara hiyo leo Machi 19,2020, kwa kukagua utekelezaji wa miradi hiyo ya maji yanayotoka Ziwa Victoria, kwa usimamizi wa Wakala wa Maji Vijjini (RUWASA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA).
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo ya maji, Mboneko amewataka wananchi ambao wanatekelezewa miradi hiyo waitunze miundombinu yake na kutoiharibu, ili idumu kwa muda mrefu pamoja na kuwaondolea adha ya kutumia maji ambayo siyo salama kwa afya zao.
Amesema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kutekeleza miradi ya maji kwa wananchi, hivyo ni vyema miradi hiyo wakaitunza huku akiwataka wasimamizi wa vituo vya kuchotea maji wawepo muda wote ili wananchi wasikose huduma ya maji hata mara moja.
“Leo nimefanya ziara ya kukagua miradi hii ya maji ambayo inatekelezwa kwa fedha za Serikali katika eneo la Uzogole, Lubaga, pamoja na Masengwa ili kuona inaendeleaje na wananchi waanze kutumia huduma hii ya maji safi na salama, maji kutoka Ziwa Victoria,” amesema Mboneko.
“Na kwenye vituo vya kuchotea maji mfano hapa Lubaga ambapo mradi umeshakamilika na kuanza kutoa maji, wasimamizi wa kituo hicho wauze maji kwa kufuata bei elekezi ya Serikali Shilingi 25 kwa ndoo moja, na siyo kuzidisha na uongozi usome mapato na matumizi kwa wananchi,”ameongeza.
Pia amemtaka mkandarasi anayejenga mradi wa maji Masengwa (Emirates Bulder) aongeze kasi ya utandazaji wa mabomba ya maji pamoja na ujenzi wa tenki la maji, ili mradi huo ukamilike haraka na wananchi waanze kutumia maji safi na salama.
Aidha amempongeza mkandarasi huyo kwa kutekeleza agizo la Serikali, la kununua vifaa vya kutekelezea mradi huo wa maji Masengwa kutoka ndani ya nchi jambo ambalo litakuza uchumi wa nchi.
Naye Kaimu Meneja Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) wilaya ya Shinyanga Emmael Mkopi, alisema katika mradi wa maji Uzogole, ulianza Februari mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Aprili 15, 2020 kwa gharama ya Shilingi Milioni 150, ambap mradi wa Masengwa ulianza Juni 2018 na utakamilika Aprili 27 mwaka huu na umegharimu Shilingi Bilioni 4.19.
No comments: