LIVE STREAM ADS

Header Ads

Umoja wa Taasisi za Dini watekeleza miradi miwili ya kijamii Buchosa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Edwin Soko, Buchosa
Umoja wa Taasisi za Dini (TIP) unatekeleza miradi miwili ya kijamii katika Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema kwa lengo la kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI na ukatili wa kijinsia kwa watoto.

Afisa Ufuatiliaji na Tathimini wa Mradi wa Boresha, Amina Ally anasema miradi hiyo inalenga kutoa elimu kwa viongozi wa dini ili waweze kuielimisha jamii kuwa na tabia ya kupima virusi vya UKIMWI kwa hiari na pia kuepusha unyanyapaa kwa waathirikia wa UKIMWI.

Aliongeza kuwa mradi wa pili unalenga kutoa elimu kwa viongozi wa dini juu ya kupinga ukatili wa kingono kwa watoto na kwamba miradi hiyo ilisainiwa mwaka 2019 huku utekelezaji wake ukianza rasmi mwaka huu 2020.

Naye Meneja Mradi huo Buchosa, Asina Shenduli ambaye pia ni Mwakilishi wa BAKWATA alibainisha kuwa matarajia ni kuona elimu ya UKIMWI inatolewa na viongozi wa dini kwa waumini wao kupitia mfumo wa ujumbe mpya wa matumaini (New Message of hope) ili waumini wao wapate tumaini jipya hata kama wanaishi na maambukizi ya VVU wajitokeze kupima na kutumia dawa kikamilifu.

Alibainisha kuwa mradi wa kupinga ukatili wa kingono kwa watoto pia viongozi wa dini wanatumika kuibua ukatili wa kingono kwa watoto na kuufuatilia hadi hatua zichukuliwe kwa wahusika.
Naye Salimu Imbwe ambaye ni Afisa wa Utekeleza Mradi huo Buchosa, alisema kuwa katika kuhakikisha mradi wa BORESHA unatekelezwa na kufanikiwa wanafanya kazi na wadau mbalimbali ambao ni wasaidizi wa kisheria, Afisa Ustawi na Maendeleo wa Buchosha, Dawati la Jinsia Buchosa na viongozi wa dini Buchosa.

Kwa upande wake Kassim Khamis ambaye ni Mratibu wa Programu Buchosa alisema licha ya mradi huo kuanza kutekelezwa mwaka huu, baadhi ya mafanikio yameanza kuonekana na TIP itaendelea kufanya kazi kwa kuhusisha wadau wake.

Taasisi zinazounda TIP ni nne ambazo ni Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT) na Ofisi ya Mufti Zanzibar.

Eneo jingine la utekelezaji wa mradi ndani ya Mkoa wa Mwanza ni Wilaya ya Ilemela na Wilaya ya Kwimba. SOMA>>> Habari zaidi kutoka Buchosa

No comments:

Powered by Blogger.