LIVE STREAM ADS

Header Ads

Maadhimisho ya Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia yanoga mkoani Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Shirika la kutetea haki za wasichana na wanawake KIVULINI kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo jeshi la polisi, limeratibu maadhimisho ya Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia yanayofanyika kwa Mkoa Mwanza katika uwanja wa Furahisha. 

Maadhimisho hayo yameanza Jumatano Novemba 25, 2020 yakitanguliwa na maandamano ya amani yaliyowashirikisha wadau na wanaharakati mbalimbali wa masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa lengo la kufikisha elimu katika jamii kupitia mabango. 

Akizunumza kuhusiana na maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally amewataka wazazi na walezi kutojikita kwenye majukumu na kusahau malezi bora ya watoto wao hususani mabinti. 

Amesema ubize wa wazazi na walezi katika jamii umechangia ongezeko la mimba na ndoa za utotoni na hivyo kuwanyima fursa ya kuhitimu masomo ambapo ametoa rai kwa wanafunzi wa kike hususani waliochaguliwa kuendelea na masomo ya vyuo vikuu kutulia na kutoweweseka na “engagement tegesha” kwani zimekuwa na madhara makubwa vyuoni. 

“Hivi sasa limeibuka wimbi la wanaume matapeli, wanawavalisha pete za kutegesha wanakimbilia kuposti status mitandaoni lakini baadae wanaachwa, wapunguze muweweseko wa engagement tegesha pamoja na zawadi za birthday, wataishia kupigwa” amesisitisha Yassin. 

Maadhimisho ya Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia hufanyika kila mwaka kuanzia Novemba 25 hadi Disemba 10 ambapo wadau na mashirika mbalimbali hutumia fursa hiyo kutoa elimu kwa jamii ili kutonyamazia aina zote za ukatili wa kijinsia.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Tazama picha za jumbe na wadau mbalimbali wakiwa kwenye maandamano ya Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijisia mkoani Mwanza yaliyoanzia viunga vya Gandhi (Gandhi Hall) kuelekea uwanja wa Furahisha.
Tazama BMG ONLINE TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.