LIVE STREAM ADS

Header Ads

MWANZA: Watoto zaidi ya 200 waliokuwa mitaani warejeshwa nyumbani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Shirika la Railway Children limefanikiwa kuwarejesha nyumbani watoto 272 waliokuwa wanaishi mitaani katika Jiji la Mwanza kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2018/20 huku pia likihakikisha wanaendelea na masomo.

Meneja Mradi wa Shirika hilo, Abdallah Issa aliyasema hayo wakati wa ziara ya waandishi wa habari kuwatembelea baadhi ya watoto na vijana walionufaika na shirika kupitia mradi wa Kivuko.

Issa alisema kupitia mradi huo wa Kivuko ulioanza Machi 2018 ukitarajiwa kuisha Machi 2021, shirika pia limefanikiwa kuwasaidia vijana 221 waliokuwa wanaishi mitaani kwa kuwajengea uwezo wa kujitambua, kuwaunganisha na taasisi mbalimbali za mafunzo ikiwemo magari ili kupata ujuzi wa kusaidia kujitegemea kiuchumi.

Aliongeza kuwa shirika pia limefanikiwa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa watoto na vijana zaidi ya 500 waliokuwa wanaishi mitaani huku matarajio yakiwa ni kuwaunganisha na familia zao watoto zaidi ya 200 ifikapo mwezi Disemba mwaka huu 2021.

“Lengo ni kuendelea kuwarejesha nyumbani watoto wanaoishi mitaani, kuwapatia mafunzo na elimu ya kujitambua ambapo pia tumefanikiwa kuwarejesha baadhi ya watoto shuleni na kugharimia mahitaji yao” alibainisha Issa.

Baadhi ya watoto katika kituo cha kutwa cha kulelea watoto wanaoishi mitaani ‘Kivukoni Smart School’ walikiri kutamani kurejea makwao kutokana na changamoto wanazozipata mitaani ikiwemo usalama mdogo, kukosa chakula na malazi.

“Tunakuja hapa asubuhi, tunafundishwa, tunacheza na kupata chakula kisha mchana tunarudi mtaani” alieleza mmoja wa watoto huku akilishukru shirika la Railway Children kwa namna linavyowasaidia.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Baadhi ya vijana wa kiume wanaopata mafunzo ya ufundi magari kwa ufadhili wa shirika la Railway Children wakiendelea na mafunzo yao.
Mmoja wa vijana wa kike aliyenufaika na mafunzo pamoja na mtaji kutoka shirika la Railway Children akiwa kwenye eneo lake la biashara katika eneo la stendi ya mabasi jijini Mwanza. BONYEZA HAPA KUONA SIMULIZI YAKE
Meneja Mradi wa shirika la Railway Children, Abdallah Issa akielezea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na shirika hilo katika kuwasaidia watoto na vijana wanaoishi mitaani.
Shirika hilo linatekeleza shughuli zake katika mikoa ya Mwanza, Dar es salaam, Arusha, Dodoma, Mbeya na Iringa.

No comments:

Powered by Blogger.