LIVE STREAM ADS

Header Ads

Ahadi ya Hayati Magufuli kwa wananchi wa Morogoro kutimizwa kwa wakati

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Nkolante Ntije (wa kwanza kulia), alipokuwa akikagua Daraja la Mto Ruvu eneo la Kibungu Chini katika barabara ya Bigwa hadi Kisaki (km. 133.6).
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro Mhandisi Nnkolante Ntije (wa pili kutoka kulia), wakati akikagua barabara ya Bigwa hadi Kisaki,eneo la Bigwa – Kiswira/Msalabani km 50, inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya (kushoto), pamoja na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro Mhandisi Nnkolante Ntije (kulia), wakiangalia hali ya Daraja la Mto Ruvu (halipo pichani), katika barabara ya Bigwa hadi Kiswira urefu wa km 50 inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami.
Muonekano wa Daraja la Mto Ruvu, eneo la Kibungo Chini katika barabara ya Bigwa hadi Kiswira km 50 ambalo litaondolewa na kujengwa daraja jipya litakalo kuwa na uwezo wa kupitisha magari pande zote mbili kwa wakati mmoja.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya akipokea zawadi ya matunda aina ya mashelisheli kutoka kwa mkazi wa Kijiji cha Matombo eneo la Msalabani, mkoani Morogoro, mara baada ya kukagua barabara ya Bigwa hadi Kiswira yenye urefu wa km 50 itakayojengwa kwa kiwango cha lami.


Na Baltazar Mashaka, Morogoro
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imesema ahadi ya ujenzi wa barabara ya Bigwa hadi Kisaki, kwa kiwango cha lami iliyotolewa na aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli mkoani Morogoro itatekelezwa haraka ili kumuenzi.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alipotembelea na kukagua barabara ya Bigwa hadi Kisaki yenye urefu wa km 133.28.

Barabara hiyo tayari ilikwisha kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, tangu mwaka 2017 na Kampuni ya Mshauri M/s Unitec Civil Consultant ya Tanzania tangu mwaka 2017 ikishirikiana na Kampuni ya Multi Tech (PTY) Ltd ya nchini Botswana.

Akizungumza na waandishi wa habari katika daraja la Mto Ruvu, eneo la Kibungo Chini, Kasekenya alisema amefika katika barabara hiyo ya Bigwa-Kisaki kufuatia ahadi ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ya kuijenga kwa kiwango cha lami barabara hiyo yenye urefu wa km 40 .

Alisema kuwa Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki,Hamis Taletale alimuomba Rais Dk. Magufuli kuijenga kwa kiwango cha lami kutoka na umuhimu wake kwa wakulima na kwa uchumi wa Morogoro.

"Itakumbukwa kuwa Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Hamisi Taletale alimuomba Hayati Dkt. Magufuli alipokuwa akifungua Soko la Kingalu, Februari mwaka huu, kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami kutokana na umuhimu wake kwa wananchi na wakulima wa Mvuha,Matombo na maeneo jirani katika usafirishaji wa mazao ya chakula, matunda na mbogamboga, lakini pia ni barabara pekee inayoiunganisha Mkoa wa Morogoro na Stesheni ya Tazara ya Kisaki,”alisema Mhandisi Kasekenya.

Alisema kuwa, ahadi za Hayati Dk. Magufuli zinaendelea kutekelezwa chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kama ambavyo amekuwa akijipambanua kupitia salamu yake na kauli mbiu yake isemayo “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi iendelee” na ni kweli kazi zinaendelea kutekelezwa, hazitasimama.

Pia alisema Daraja la Mto Ruvu, eneo la Kibungo Chini katika barabara ya Bigwa hadi Kiswira km 50 litaondolewa na kujengwa daraja jipya litakalo kuwa na uwezo wa kupitisha magari pande zote mbili kwa wakati mmoja.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro,Mhandisi Nkolante Ntije, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, ofisi yake iko tayari kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ya Bigwa hadi Kisaki sehemu ya Bigwa hadi Kiswira urefu wa km 50 badala ya km 40 za awali kufuatia maombi ya Serekali ya Mkoa wa Morogoro.

“Niwatoe hofu wananchi wa maeneo yaliyopitiwa na mradi huu kwakuwa hautachukua muda mrefu hivyo basi wajiandae na wasiwe na wasiwasi kwa sababu sheria, kanuni na taratibu za fidia zitafuatwa kwa maeneo ambayo yalikuwa nje ya hifadhi ya barabara yatakayotwaliwa ili kupisha mradi huu,” alisema Mhandisi Ntije.

Naibu Waziri huyo wa Ujenzi na Uchukuzi,Mhandisi Kasekenya yuko mkoani Morogoro kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ili kukagua miundombinu ya barabara iliyoharibika kutokana na mafuriko yayaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.

No comments:

Powered by Blogger.