LIVE STREAM ADS

Header Ads

Balozi wa Marekani aipongeza Klabu ya Waandishi wa Habari Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Tony Alphonce, Mwaza
Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kupitia kwa Balozi wake, Donald Wright umeipongeza Klabu ya Waandishi wa Habari ya Mkoa Mwanza (MPC) kwa kuandaa kongamano la mtandaoni kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani iliyoadhimishwa Mei 03, 2021

Balozi Wright ametoa pongezi hizo wakati akitoa hotuba yake ya tathimini ya hali ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwenye kongamano hilo lililoandaliwa kwa ushirikiano baina ya MPC na Shirika la kimataifa la Internews.

Wright alisisitiza kuwa kilele cha maadhimisho hayo ni kielelezo cha vyombo vya habari kufanya kazi kwa maslahi ya jamii bila kuingiliwa. na kuongeza kuwa vyombo vya habari vikiwa huru vinajenga jamii imara yenye kujiamini kwani inakuwa na nafasi ya kusema lolote linaloihusu jamii.

Alisema maadhimisho hayo ni muhimu kwa kuwa pia yanalenga kukumbushana juu ya wajibu wa vyombo vya habari kwenye kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha jamii.

"Vyombo vya habari lazima viendane na mabadiliko na ukuaji wa teknolojia ili iweze kubuni mbinu mpya za kibishara na uwekezaji, Marekani ina programu mbalimbali za kufanya kazi na wamiliki wa vyombo vya habari ili kuleta tija kwenye biashara" alieleza Balozi Wright.

Naye Mwenyekiti wa MPC, Edwin Soko alimshukuru Balozi Wright kwenye hotuba yake kwa kuamua kusherehekea kwa pamoja maadhimisho ya mwaka huu na wanahabari wa Tanzania.

"Siku ya leo ni siku ya kutafakari namna bora ya kufanya kazi zetu kwa kuzingatia usalama pamoja na tija kwa jamii ili kujenga jamii bora" Alisema Soko.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na zaidi ya washiriki sitini kutoka kwenye vyombo vya habari mbalimbali pamoja na wanazuoni yakienda pamoja na kauli mbiu isemayo "Habari kwa Manufaa ya Umma.

Wakati maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika hali ya ukiukwaji wa haki za waandishi umeongeza ambapo kwa mujibu wa tafiti kutoka Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka kwa mwaka 2020 waandishi wa habari zaidi ya 50 waliuawa huku 274 wakifungwa.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald Wright.

No comments:

Powered by Blogger.