LIVE STREAM ADS

Header Ads

KATAMBI: Siyo ushamba Baba kumlea mtoto wako

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Wazazi wa kiume nchini (akina baba) wametakiwa kutenga muda kwa ajili ya malezi ya watoto wao na kuacha tabia ya kuwaachia majukumu yote wazazi wa kike (akina mama).

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Patrobasi Katambi alitoa rai hiyo Juni 20, 2021 wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Baba Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Shinyanga ikiwa ni mara ya kwanza kuadhimishwa nchini.

Katambia alisema pamoja na wanaume kuhakikisha familia inapata mahitaji muhimu, bado wana jukumu la kuwa karibu na watoto kwa kuwaonyesha upendo wa dhati huku akiwataka kuondokana na dhana kwamba akina baba kulea watoto ni ushamba.

"Watoto wanawapenda mama zao siyo uchawi ni kwa sababu wapo karibu nao tofauti na akina baba. Sisi muda tunaokuwa karibu na watoto ni ule wa matukio mabaya tu hali inayopelekea mtoto kumuona baba ni katili na wakati wa matukio yote mazuri kina baba hatushiriki tunawaachia kina mama, hii inasababisha mtoto kugawa upendo" alisema Katambi.

Aidha Katambi aliwataka wanaume wote nchini kutumia maadhimisho hayo kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuheshimu mchango unaotolewa na wanawake katika malezi na makuzi ya mtoto katika jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Leticia Mourice alisema Baraza hilo linaadhimisha Siku ya Baba Duniani likimwangalia baba kama muhimiri wa familia huku akiwa na mama pamoja na mtoto anayeishi na maambukizi ya VVU.

Alisema baba ananafasi kubwa ya kuhakikisha mama au mtoto anayeishi na VVU anapata huduma zote muhimu ikiwemo uhuru wa kutumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI bila kificho.

Aliwataka wanaume wa Mkoa wa Shinyanga na Tanzania kwa ujumla kuwa mstari wa mbele katika kupinga vitendo vya unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU huku akikemea kitendo cha ukatili kilichofanywa na baba kuwaua mama na mtoto baada ya kugundua anatumia ARV.

"Hakikisheni kitekohiki hakijirudii, wanaume wawe mstari wa mbele kumsaidia mama au mtoto mwenye VVU kupata huduma zote muhimu" alisisitiza Mourice.
Maadhimisho ya Siku ya Baba Duniani 2021 yaliandaliwa na Serikali mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) pamoja na shirika la ICS Afrika.
Na Tonny Alphonce, Shinyanga

No comments:

Powered by Blogger.