LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shinyanga wachukua hatua kufanikisha zoezi la utoaji Chanjo ya Uviko 19

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dr. Philemon Sengati amewaagiza wakuu wa wilaya kumshughulikia mtu yeyote atakayepotosha kuhusu chanjo ya UVIKO-19 ndani ya Wilaya za Mkoa wa Shinyanga kwani mtu huyo hautakii Mkoa maendeleo huku akitoa siku 20 kutekeleza mpango shirikishi na harakishi kuhusu utoaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19.

Dkt. Philemon Sengati alitoa agizo hilo Septemba 27,2021 wakati akifungua kikao kwa ajili ya Mafunzo kwa wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi mkoa wa Shinyanga (PHC) ya utekelezaji wa mpango shirikishi na harakishi kuhusu utoaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19.

Kikao hicho kimekutanisha wadau mbalimbali wa afya kwa ajili ya kuwajengea uwezo na uelewa juu ya chanjo ya UVIKO-19 na namna ya kufanya uhamasishaji kwa jamii kuhakikisha walengwa wengi kwa chanjo wanafikiwa na hatimaye kupunguza maambukizi na kukinga dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.

“Mtu yeyote atakayepotosha kuhusu chanjo ya UVIKO-19 ndani ya Wilaya za Mkoa wa Shinyanga basi Wakuu wa Wilaya mumshughulikie mtu huyo kwani hautakii Mkoa maendeleo” alisema Dkt. Sengati.

Dkt. Sengati alisema kutokana na muitikio mdogo serikali imekuja na mpango mkakati unaoitwa Mpango Shirikishi na Harakishi wa utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 ili kufikia malengo ya asilimia 100 ya chanjo zote zilizopokelwa zitolewe kwa wananchi ndani ya siku 20 tulizojiwekea kama Mkoa kuanzia tarehe 01 Oktoba, 2021 hivyo hatapenda kuona mtu yeyote anapotosha kuhusu chanjo.

“Tunapofanya ufunguzi rasmi wa utekelezaji wa Mpango Shirikishi na Harakishi wa Chanjo dhidi ya UVIKO-19 naomba Chanjo iwe kipaumbele kwa kila mmoja wetu hivyo Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya na viongozi mbalimbali na wadau wote mshiriki na kusimamia zoezi hili na kuhakikisha kila mwananchi mwenye umri kuanzia miaka 18 anahamasika na kupatiwa chanjo” alisema Dkt. Sengati.

Aliwashauri viongozi kuwa mstari wa mbele kujitokeza kuchanja na kuhamasisha wananchi kuchanja ili wananchi waendelee kuwa imara zaidi akibainisha kuwa kuanzia kesho atafanya ziara kwenda kwenye maeneo ya kimkakati ili kuondoa mitazamo hasi kuhusu chanjo ya UVIKO - 19.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Kalidushi Charles alisema wameamua kuja mkoani Shinyanga kuja kuongeza nguvu katika utoaji chanjo kwani mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa 10 ya mwisho kwa idadi ya watu waliochanjwa hadi kufikia Septemba 25,2021. Mingine ni Lindi, Singida,Geita, Manyara, Rukwa, Simiyu, Njombe, Katavi na Songwe.

Alizitaja fursa zilizopo kwa ajili ya chanjo maeneo yanayotakiwa kupelekewa chanjo kuwa ni machimbo,masoko, stendi za mabasi,nyumba za ibada, viwanda, vikao na makongamano mbalimbali, taasisi mbalimbali za umme na za binafsi, vyama vya siasa, vijiwe vya bodaboda,majeshi, watoa huduma za asili na watu maarufu.

Aliwaomba viongozi wa dini wahamasishe kwenye makanisa na misikiti ili waumini wao waweze kupata chanjo na waruhusu wahudumu kwenda kutoa huduma za ibada.

“Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa wilaya wanapokuwa kwenye maeneo ya wananchi kwa shughuli mbalimbali waongelee habari ya chanjo na waambatane na wahudumu wa afya wakiwa na chanjo. Pia wakuu wa wilaya wawaelekeze watendaji walio chini yao kushiriki kikamilifu katika zoezi la uhamasishaji na uchanjaji” alisema.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile alisema zoezi la uchanjaji Chanjo ya UVIKO -19 lilianza Agosti 4,2021 na hadi kufikia Septemba 26,2021 jumla yaa chanjo zilizotumika ni 6,990 sawa na asilimia 28 ya chanjo zote 25,000 zilizotolewa mkoani Shinyanga ambapo jumla ya watu waliopata chanjo ni 6,027.

“Jumla ya watu waliopata chanjo hadi kufikia Septemba 26,2021 katika Manispaa ya Shinyanga ni 2445, Manispaa ya Kahama 1863, Halmashauri ya Kishapu 651, Msalala 640, Shinyanga 312 na Ushetu 116” alieleza Dkt. Ndungile.

“Katika siku 54 za utoaji chanjo Wanaume wameongoza kuchanja chanjo ambapo jumla ya wanaume 4015, Wanawake ni 2012 hivyo kuna umuhimu wa kuhamasisha wanawake kujitokeza kuchanja" alisema.

Alisema zoezi la utoaji vyeti vya Kielektroniki kwa watu waliochanjwa chanjo ya UVIKO – 19 linaendelea vizuri.

Nao Wadau wa afya walioshiriki kwenye kikao hicho walisema "Chanjo ni muhimu sana kwa mustakabali wa kiuchumi wa taifa na unapochanjwa unakuwa imara,utakuwa na nguvu ya kuhimili ugonjwa huo ili uweze kuendelea kutekeleza majukumu yako".
Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akifungua Kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Shinyanga kinachohusu uhamasishaji wa Chanjo ya UVIKO-19.
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Kalidushi Charles akizungumza kwenye kikao hicho.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Yudas Ndungile akizungumza kwenye kikao hicho cha Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Shinyanga.
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Kalidushi Charles akizungumza kwenye kikao hicho.
Mratibu wa Chanjo ya UVIKO - 19, Timoth Sosoma akizungumza kwenye kikao hicho.
Wadau wa afya wakiwa kwenye kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Shinyanga kinachohusu uhamasishaji wa Chanjo ya UVIKO-19.
Wadau wa afya wakiwa kwenye kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Shinyanga kinachohusu uhamasishaji wa Chanjo ya UVIKO-19.
Wadau wa afya wakiwa kwenye kikao hicho.
Wadau wa afya wakiwa kwenye wakifuatilia kikao hicho.
Wadau wa afya wakiwa kwenye kikao hicho cha Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Shinyanga kinachohusu uhamasishaji wa Chanjo ya UVIKO-19.
Wadau wa afya wakiwa kwenye kikao cha Kamati hicho.
Wadau wa afya wakifuatilia kikao hicho.
Wadau wa afya wakiwa kwenye kikao hicho cha Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Shinyanga kinachohusu uhamasishaji wa Chanjo ya UVIKO-19.

No comments:

Powered by Blogger.