LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kampuni ya Lake Oil matatani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Dkt. Samuel Gwamaka ameitoza faini ya shilingi Bilion 3.3 (bilioni Tatu na milioni miatatu) Kampuni ya Lakeoil kwa kosa la kutokufuata Sheria na Kanuni za kuanza au kufanya mradi bila kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira.

Ameyasema hayo alipokuwa katika mkutano na waandishi wa habari katika Ofisi za NEMC Makao Makuu, jijini Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na kuwataka wenye miradi kufanya Tathmini ya athari kwa Mazingira kabla ya kufanya au kuanza miradi.

‘’ Mimi Mkurugenzi wa Mazingira, kupitia Kifungu cha 196 (1,2,3 na cha 4) naipa adhabu Kampuni ya Lakeoil Limited, namtoza faini ya shilingi bilioni 3.3 (bilioni tatu na milioni mia tatu) kwa kosa hilo, ambazo nataka azilipe ndani ya siku 14(kumi na nne) kuanzia kesho tarehe 7/9/2021. Asipofanya hivyo vituo vyote 66 (sitini na sita) vya Lakeoil ambavyo havina Tathmini ya Athari ya Mazingira tutavifungia visifanye kazi.’’-Dkt.Samuel Gwamaka.

Aidha amesema Baraza litaendelea kufuatilia vituo vingine vya kampuni nyingine ambazo hazijafanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na vyenyewe vitatozwa faini kwa mujibu wa Sheria hivyo,

‘’Natoa rai yeyote mwenye vituo vya mafuta au mradi wa Tathmini ya Athari ya Mazingira au mwenye cheti cha Enviromental Audit ajisalimishe ndani ya siku 7 (saba) kwenye ofisi za Baraza la Mazingira Taifa. Kwa mradi wowote ambao umeanza kazi baada ya 2004 na mradi wowote ambao umekuwa ukifanya kazi kabla ya 2004 ambao haujafanya Environmental audit wajisalimishe ndani ya siku 7 (saba), baada ya hapo sheria itachukua mkondo wake tutawaadhibu wote kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira.’’-Dkt. Samuel Gwamaka.

Aidha alimaliza kwa kusema miaka 17(kumi na saba) imepita toka Sheria imewekwa, jamii imeelimishwa vya kutosha,

‘’Elimu imetolewa sana na Baraza na wadau mbalimbali, uhamasishaji umefanyika sana kuwataka watu waweze kufanya ukaguzi wa mazingira lakini pia baraza limejitahidi kusambaza huduma nchi nzima ili wadau waweze kufikia ofisi zetu waweze kusajili miradi ili kukidhi haja na matakwa ya mazingira haswa ambayo yamewekwa kwenye sheria ya mazingira ya mwaka 2004. Sasa ni Sheria kuchukua mkondo wake.
Na Adam Sayi, Dar

No comments:

Powered by Blogger.