Waziri Gwajima afunguka mafanikio ya Wizara ya Afya kuelekea miaka 60 ya Uhuru
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima, akitoa taarifa ya Mafanikio ya Sekta ya Afya kuelekea miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika itakayosherekewa Desemba, 09, 2021.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima, akitoa taarifa ya Mafanikio ya Sekta ya Afya kuelekea miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika.
Makatibu Wakuu Wakuu wa Wizara ya Afya pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo, wakiwa wanafatilia taarifa ya Waziri Gwajima jijini Dodoma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima, akitoa taarifa ya Mafanikio ya Sekta ya Afya kuelekea miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika itakayo sherekewa Desemba, 09, 2021, huku waandishi wakiwa kazini kuchukua tukio hilo.
NA WAMJW
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (Mb), amesema Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye Sekta ya Afya, wakati huu Nchi inapoelekea kusherekea Miaka 60 tangu ipate Uhuru, huku akisifu Jitihada za Uongozi tokea awamu ya kwanza ya hayati Baba wa Taifa Mw. JK. Nyerere, hadi awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa sasa.
Akizungumza na vyombo vya Habari Novemba 08, 2021, Dkt. Gwajima amesema mara tu baada ya kupata Uhuru, aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitamka bayana kwamba, Maradhi ni miongoni mwa maadui wa maendeleo na ivyo kila mmoja mtanzania alipaswa kusimama imara katika kukabiliana na adui maradhi.
“Mafanikio ya miaka 60 baada ya uhuru ni mengi, mathalani, vituo vya kutolea huduma za afya ngazi zote imeongezeka hadi kufikia vituo 8,537 ikilinganishwa na vituo 1,343 Mwaka 1960. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 84.26. Aidha, kati ya vituo hivyo, Serikali inamiliki asilimia 64, Mashirika ya dini asilimia 9 na vituo binafsi asilimia 27” alisema Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima amesema kuwa, Mtandao wa vituo vya huduma za afya umepanuka na kusogea karibu zaidi na wananchi ambapo kwa sasa zahanati ni 7,242; vituo vya afya 926; na Hospitali za Wilaya ni 178, Hospitali zingine ni 151. Aidha, hospitali za kibingwa ngazi ya mikoa ni (28), ngazi ya Kanda Sita (6), hospitali za ubingwa maalumu ni Tano (5) na hospitali ya taifa ni moja (MNH).
Waziri Gwajima, amesema, Vituo vyote hivi vina jumla ya vitanda 90,488 ikiwa ni sawa na ongezeko la vitanda 71,656 sawa na asilimia 79.18. Kwa sasa uwiano wa vituo kwa idadi ya watu ni kituo kimoja kwa watu 6,751.5 (1: 6,751.5) tofauti na kabla ya Uhuru na 1:40000-50000 kabla ya uhuru. Hatua hii inaifanya Tanzania kufikia malengo ya umoja wa mataifa katika upatikanaji wa huduma za afya kwa kuzingatia idadi ya watu na Jiografia.
Waziri Gwajima, amefafanua kuwa, uwiano wa vitanda kwa idadi ya watu ni kitanda kimoja kwa watu 637 (1:637) ukilinganisha na 1:1000 kabla ya uhuru mpaka mwaka 2020 uwiano wa wagonjwa kwa vitanda umekuwa kitanda kimoja kwa watu 19 (1:19).
Mafanikio mengine, ambayo yamewekwa bayana na Waziri Dkt. Gwajima ni juu ya idadi ya watumishi na wigo wa kada za wataalamu kwenye vituo vya kutolea huduma, amabapo amesema umepanuka kiasi kwamba hivi sasa vituo vya afya vinafanya hadi huduma za upasuaji mkubwa ambao apo awali ulikuwa haufanyiki.
“Tunapoelekea kusherekea Miaka 60 ya Uhuru, Idadi ya wataalamu wa baadhi ya kada mbalimbali za msingi kwenye afya waliosajiliwa imeongezeka hadi kufikia zaidi takribani 71,365, kada zinazojumuisha madaktari bingwa, wa kawaida, wauguzi, wataalamu wa maabara, mionzi, wafamasia na mionzi. Kabla ya uhuru wote hawa kwa ujumla walikuwa 435 tu hii ni hatua kubwa sana ka nchi tumepiga” amesema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wa chanjo mbali mbali, Waziri Gwajima amesema huduma hiyo imeimarika na kufanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazotekeleza kwa ufanisi eneo hilo hususan chanjo za watoto chini ya mwaka mmoja (1) huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 101. Sambamba na kila kituo cha huduma za afya kuwa na huduma ya chanjo kwa ajili ya Kinga ya ugonjwa wa Polio (OPV3), PENTA-3 kwa ajili ya kuzuia magonjwa ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda (tetanus), homa ya ini na homa ya uti wa mgongo na chanjo ya Surua/ Rubella.
Waziri Gwajima alitumia fursa hiyo kuelezea juhudi za sasa chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na kazi ya kuboresha huduma za afya hususan suala la UVIKO-19, ambapo amesema, juhudu za Rais zimewezesha Nchi kupata mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Kimarekani milioni 567.25 sawa na Shilingi trilioni 1.362 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambapo, tarehe 10 Iktoba, 2021 wakati akizindua kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO – 19 alitenga Shilingi Bilioni 466.781 (34%) kwa ajili ya Sekta ya Afya.
Fedha hizo ziliekezwa kwenye maeneo kama ifuatvyo, uimarishaji wa huduma za dharura, Shilingi bilioni 254.4, huduma za maabara, mionzi na tiba mtandao; itakayogharimu Shilingi bilioni 111.5 huduma za chanjo dhidi ya UVIKO - 19 na elimu ya afya kwa umma dhidi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo, itakayo gharimu Shilingi bilioni 43.2 vilevile, uimarishaji wa miundombinu katika vituo vya kutolea huduma za Afya itakayogharimu Shilingi bilioni 41.8 pamoja na kufanya tafiti za kitaalam kuhusu Virusi vya Korona pamoja na kuwajenga uwezo watoa huduma za Afya; itakayogharimu Shilingi bilioni 15.9.
Akiwa anahitimisha taarifa yake mbele ya Vyombo vya Habari, Dkt. Gwajima, alisema Serikali imepiga hatua kubwa katika mchakato wa ukamilishaji wa Rasimu ya Bima ya Afya kwa wote, kufuatia swali la Mwandishi wa gazeti la Mwananchi Abel Chidawali aliyetaka kujua hatua ya rasimu hiyo.
Taarifa kwa vyombo vya Habari ni mfululizo wa Wizara kutoa taarifa, mpango unao ratibiwa na Idara ya Habari Maelezo kwa Ushirikiano na Vitengo vya Mawasiliano Serikalini ndani ya Wizara na taasisi, kuelekea miaka 60 ya Uhuru.
No comments: