LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Gwajima ataka changamoto za watoto wanaoishi mtaani zitafutiwe ufumbuzi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Na WMJJM, Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amewaasa wadau wote kushirikiana ili kuhakikisha changamoto za watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani zinapatiwa ufumbuzi.

Waziri Gwajima ametoa rai hiyo Januari 25, 2022 alipotembelea makao ya kulea watoto yatima na wazee wasiojiweza yanayoendeshwa na Watawa wa Upendo yaliyopo Hombolo mkoani Dodoma.

Alisema bado kuna watoto wengi wanaoishi na kufanya kazi Mitaani na Serikali kwa kushirikiana na Wadau bado inatafuta ufumbuzi.

"Tukumbuke watoto wanaoishi Mitaani wanakutana na changamoto nyingi ikiwemo ukatili, ukatili wa majumbani ni sababu na matokeo yake wanakutana na mazingira hatari zaidi hii haikubaliki" alisema Waziri Gwajima.

Akifafanua kuhusu takwimu, Dkt. Gwajima, alisema. asilimia 70 ya watoto wanaoathirika na ukatili ni watoto wa kike, huku Idadi wanawake ikitajwa kufikia
asilimia 96.

"Ili tuweze kupunguza kadhia hii, silaha ya kwanza ya jamii ni uelewa wa pamoja na kukataa kwa Nguvu moja, kuweka mifumo madhubuti ya kuzuia vitendo vya ukatili" alisema Gwajima.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mwanaidi Ali Khamis akizungumza na walezi wa makao hayo, aliwataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuamka na kufanya kazi yao waliyokusudiwa.

Akizungumza wakati wa Ziara hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Zainab Chaula aliitaka jamii kutumia rasilimali zilizopo maeneo yao kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo kuongeza kipato na kuwasaidia wahitaji, huku akitolea mfano Bwawa la Hombolo na wewe jinsi linavyoweza kuwa mkombozi.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo mpya, Amon Mpanju alitoa rai kwa wananchi kuwa na moyo wa kujitolea kuwasaidia wahitaji kwa namna mbalimbali.

Wakati wa Ziara hiyo Diwani kata ya Hombolo,Mhe. Mathayo Ndajiro hakuacha kuipongeza Wizara kwa mikakati iliyoamua kuja nayo ikiwepo kutokomeza ukatili kwa mbinu Shirikishi kwa Makundi yote.

Awali akiwasilisha taarifa ya makao hayo kwa Waziri, Msimamizi Msaidizi wa makao hayo Mtawa Radienince MC alisema makao hayo yana uwezo wa kuhudumia watoto 40 na waliopo ni 23. Aidha Wazee wanaohudumiwa kwa sasa ni 58.

Sista Radienince aliongeza kwamba, kwa mwaka 2021 watoto wapatao 10 wameunganishwa na familia zao.

Viongozi na Menejimenti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi maalum, wapo katika ziara endelevu yakujifunza na kutafuta afua zakutatua changamoto ya Matukio ya ukatili na Ustawi wa Jamii.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, akiongea na uongozi wa Kituo cha Kule Wazee na watoto cha Hombolo jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na wanawake, Mhe. Mwanaidi Ally Khamis, akizungumza wakati wa Ziara ya Hombolo ambapo waziri wa Wizara hiyo aliongoza ujumbe huo.

No comments:

Powered by Blogger.