LIVE STREAM ADS

Header Ads

Viongozi wa dini kuelimisha wananchi umuhimu wa Anwani za Makazi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Viongozi wa Dini wanaounda Kamati ya Amani Mkoa Mwanza wamepewa elimu kuhusu anwani za makazi ili wasaidie kuwaelimisha waumini wao hatua itakayosaidia kutambua umuhimu wa anuani hizo.

Elimu hiyo imetolewa Aprili 07, 2022 kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabliel alisema viongozi wa dini wana makundi makubwa ya watu hivyo kupitia elimu hiyo watakuwa waalimu wazuri kwa waumini wao.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya kuwasaidia wananchi kuboresha mwasiliano kwenye sehemu mbalimbali ikiwemo makazi yao, sehemu zao za biashara, na maeneo mengine ya huduma za kijamii.

Naye Mratibu wa Anwani za Makazi Mkoa wa Mwanza, Abdul Mzee alisema wameamua kutoa elimu kwa Kamati ya Amani ya Mkoa inayo husisha viongozi wa dini kutoka madhehebu ya Kikristo na Waislamu kwa sababu wanaamini elimu ikifika kwa viongozi hao itafika pia kwa kila mwananchi.

Alisema kwa kipindi hiki cha mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Kwaresima, misikitini na makanisani waumini wanakuwa wengi hivyo viongozi wa dini wakitumia muda huu elimu itawafikia wananchi wengi.
Mzee alisema kwa Mkoa wa Mwanza nyumba 653,827 zimewekewa namba sawa na asilimia 118.54 ya lengo ambapo hadi sasa nyumba 421,212 zimesajiliwa kwenye mfumo wa kidigitali sawa na asilimia 64.42.

Aliongeza kuwa wanatarajia kumaliza zoezi hilo ndani ya siku saba kwani hadi sasa nguzo 6,007 zinazoonyesha majina ya barabara zimewekwa sawa na asilimia 25 ya lengo.

Aidha alisema kuwa Mkoa Mwanza unaendelea kutoa elimu ya anwani za makazi kwa makundi mbalimbali katika jamii.

Kwa upande wake Shekh wa Mkoa wa Mwanza. Hassan Kabeke ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani Mkoa Mwanza alisema mafunzo hayo yamewasaidia kufahamu namna majina ya mitaa na namba zinavyopatikana kupitia simu ya mkononi.
Aliowaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa maafisa wa anwani za makazi wapokuwa wanapita kwenye mitaa yao ili kusaidia zoezi hilo kukamilika kwa wakati.

Katika hatua nyingine Mjumbe wa Kamati hiyo, Askofu Lameck NKumba, alisema zoezi la anuani za makazi litasaidia pia utambuzi wa nyumba za ibada kutambulika kwa urahisi na kuondoa usumbufu uliokuwepo hapo awali.
Na Hellen Mtereko, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.