Mkurugenzi Jiji la Mwanza akemea tukio lililofanywa na mgambo, ameondolewa
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Askari mgambo katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza wametakiwa kufanya kazi kwa weledi wakizingatia taratibu na sheria zilizowekwa hatua itakayosaidia kutimiza wajibu wao kwa amani bila kusababisha taharuki katika jamii.
Rai hiyo imetolewa Jumamosi Apili 16, 2022 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halimashauri ya Jiji la Mwanza, Yahaya Sekiete kufuatia tukio lililosambaa kwenye mitandao ya kijamii likiwaonesha baadhi ya askari mgambo wa Jiji hilo wakirusha kwenye gari bidhaa za ndizi mbivu za mfanyabiashara mdogo waliyemkamata akifanya biashara katika eneo lisilo rasmi.
Sekiete amesema kitendo cha kutupa ndizi kwenye gari kama vile si chakula hakifai na tayari hatua za kinidhamu zimechukuliwa kufuatia tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwaondoa kwenye oparesheni askari mgambo waliohusika.
"Hata kama mfanyabiashara amekiuka utatatibu siyo vyema kuchukua bidhaa zake na kuzitupa ovyo kwani kufanya hivyo ni kukiuka maadili ya kazi" ameonya Sekiete.
Sekiete ameeleza kuwa baada ya kuwapanga wafanyabiashara wadogo katika maeneo yao maalumu, Halmashauri ya Jiji la Mwanza imeendelea na oparesheni ya kuzuia wasirejee katika maeneo yasiyo rasmi na kuwapa elimu kutofanya biashara kwenye maeneo yaliyokatazwa.
Aidha amewasihi wafanyabiashara wadogo jijini Mwanza kuendelea kufanya biashara kwenye maeneo rasmi wakizingatia kwani Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inawapenda ndiyo maana inaendelea kuimarisha masoko katika maeneo mbalimbali.
Sekiete ameongeza kuwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza inaendelea kurekebisha miundombinu katika soko la Dampo Buhongwa lengo ikiwa ni kuwatengenezea wafanyabiashara wadogo miundombinu rafiki na salama ili waweze kufanya biashara zao kwa amani na kuacha kufanya biashara barabarani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Mohamed Dauda ameeleza kusikitishwa na kitendo cha askari mgambo huyo kutupa ndizi ovyo kwenye gari akisema amefurahishwa na hatua iliyochikuliwa na Halimashauri ya Jiji la Mwanza ya kumuondoa kwenye oparesheni askari mgambo aliyehusika kuharibu bidhaa za mfanyabiashara waliyemkamata kwani itakuwa ni fundisho kwa wengine.
Aidha Dauda amewaomba wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga kufanyia biashara zao katika maeneo rasmi waliyopangiwa na Serikali ili kuepukana na changamoto ya kufukuzana na askari mgambo.
SOMA>>> Habari zaidi hapa BMG Habari
No comments: