LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Biteko atinga Busolwa Mining Mwanza, akoshwa na mfumo wa uendeshaji

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amefurahishwa na mfumo wa uendeshaji wa ubia baina ya mwekezaji mzawa kampuni ya Busolwa Mining na ushirika wa wananchi katika mgodi wa dhahabu wa Busolwa uliopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Amesema hatua hiyo ni ya mfano na inapaswa kuigwa na wawekezaji wengine nchini kwani unaondoa migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza katika maeneo yenye madini baada ya wananchi kulipwa fidia lakini mradi unapoanza uzalishaji wanaanza malalamiko.

Waziri Biteko ameyasema hayo Mei 28, 2022 baada ya kufanya ziara katika mgodi huo kukagua shughuli za uendeshaji wake ikiwemo uchimbaji na uchenjuaji dhahabu pamoja na kupokea changamoto zilizopo kwa ajili ya utatuzi.

“Kilichonifurahisha ni mfumo wa mradi huu wa kuwahusisha wananchi wa kawaida kupitia umoja wao wa Isihika ambapo wana asilimia 20 na mwekezaji kampuni ya Busolwa asilimia 80,, kuna wenzenu mwekezaji akifika wanasema wewe nipe changu, wakiulizwa shilingi ngapi wanasema yoyote uliyonayo, baada ya muda wanaanza kulalamika” amesema Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine Dkt. Biteko ameipongeza kampuni ya Busolwa Mining kwa uwekezaji mkubwa na wa kisasa ilioufanya mgodini hapo na kutoa fursa za ajira kwa watanzania pamoja na kulipa kodi serikalini ambapo kwa kipindi cha kuanzia mwishoni mwa mwaka jana hadi mwaka huu tayari imelipa zaidi ya shilingi bilioni mbili.

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan nia yake ni kutengeza mabilionea na mamilionea wapya kwa kuwapatia fursa ya kuchimba madini kwa kuwaongoza vizuri na si kutishana bali kuweka mfumo mizuri ya kila mmoja kulipa kodi na kwamba anaamini mradi huo wa Busolwa Mining utakuwa mfano wa kuigwa.

Dkt. Biteko ameomba watendaji na viongozi wa Serikali wanaosimamia sekta ya madini kuwasaidia na kuwawezesha na si kudhibiti tu wanaokosea ili wachimbaji madini waweze kufanya shughuli zao kwa amani na usalama.

Kuhusu uanzishwaji wa masoko ya madini, Dkt. Biteko amesema yamesaidia kurahisisha biashara na kupunguza changamoto ya utoroshaji madini ambapo amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu kiasi cha tani tisa ya dhahabu imeuzwa mkoani Mwanza na hivyo kuwapongeza wachimbaji kwa ushirikiano wao.

Awali Meneja Mradi Busolwa Mining, Ibrahim Nayopa ameomba Dkt. Biteko kuwasiliana na viongozi wenzake ili kusaidia utatuzi wa changamoto ya maji na umeme ambao umekuwa ukikatika mgodini hapo na kusababisha gharama za uendeshaji kuongezeka. Nayopa amesema mradi huo umetoa fursa ya ajira kwa wafanyakazi 127 pamoja na kuwanufaisha wanahisa 104 waliounda ushirika wa Isinka Federation na hivyo kuchochea maendeleo katika jamii.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Busolwa Mining, Baraka Ezekiel amesema uwekezaji wa mradi huo ni zaidi ya dola milioni 20 ambapo mitambo yake inaweza kusaga mawe ya madini kiasi cha tani 1,200 kwa siku ingawa changamoto ya umeme imekuwa ikisababisha uzalishaji kusuasua.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ushirika wa Isinka Federation, John Balole amesema mradi wa Busolwa Mining umewasaidia kuwa na uhakika wa kujipatia kipato kwa ajili ya kujikimu kimaisha huku Mkuu wa Wilaya Misungwi, Veronica Kessy akiwahakikishia wawekezaji katika mradi huo mazingira rafiki ya kufanyia kazi kwa manufaa ya pande zote mbili.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa kampuni ya Busolwa Mining, Baraka Ezekiel (kulia) baada ya kutembelea mgodi wa Busolwa
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko na ujumbe alioambatana nao akikagua eneo la machimbo ya dhahabu katika mgodi wa Busolwa uliopo Kijiji Shokelahela Kijiji cha Buhande wilayani Misungwi.
Waziri wa Madini, Dkt. Biteko na ujumbe alioambatana nao akikagua shughuli za uchenjuaji madini katika mgodi huo (Busolwa Mingi, Buhande Project) Misungwi.
Mkuu wa Wilaya Misungwi, Veronica Kessy akitoa salamu zake wakati wa ziara hiyo.
Meneja Mradi kampuni ya Busolwa, Ibrahim Nayopa akitoa taarifa ya mradi huo.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa kampuni ya Busolwa Mining na wanahisa wa ushirika wa Isinka Federation.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa kampuni ya Busolwa Mining.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.