LIVE STREAM ADS

Header Ads

Naibu Waziri wa Madini Zimbabwe atembelea kiwanda cha kusafisha dhahabu Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri wa Madini na Uendelezaji Migodi wa Zimbabwe, Dkt. Polite Kambamura ameanza ziara ya kikazi ya siku tano hapa nchini kwa lengo la kujifunza uendeshaji na usimamizi wa sekta ya madini.

Dkt. Kambamura ambaye aliwasili nchini Mei 22, 2022 ameanza rasmi ziara hiyo Mei 23, 2022 kwa kutembelea kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza (Mwanza Precious Metals Refinery) akiwa na mwenyeji wake Naibu Waziri wa Madini Tanzania, Dkt. Steven Kiruswa.

Akiwa kiwandani hapo, Dkt. Kambamura amekiri hatua kubwa iliyopigwa na Tanzania katika sekta ya madini hususani suala la uwazi katika usimamizi wa biashara ya madini pamoja na mazingira rafiki na salama kwa wafanyabiashara wa madini.

Pia Dkt. Kambamura amevutiwa na uwekezaji wa mitambo ya kisasa uliofanywa katika kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza ambacho kinamilikiwa kwa ubia baina ya Serikali na mwekezaji binafsi ambacho kina uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku kwa ubora wa asilimia 99.9.

Naye Naibu Waziri wa Madini Tanzania, Dkt. Kiruswa amesema sekta ya madini nchini imepiga hatua kubwa huku Serikali kupitia Wizara hiyo ikiweka mazingira ya kuhakikisha mawe ya madini (malighafi) ambayo hayajachakatwa na kuongezewa thamani hayauzwi nje ya nchi.

“Tunapouza madini ambayo hayajachakatwa kuna vitu vingi vyenye thamani (madini mengine) tunavipoteza hivyo kiwanda hiki ni moja ya viwanda vya kisasa katika kusafisha dhahabu Afrika ambapo Dkt. Kambamura ameona ni vyema afike hapa kujifunza” amesema Dkt. Kiruswa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya pamoja ya uendeshaji kiwanda cha kusafisha Mwanza, Deusdedith Magala amesema kiwanda hicho kina mitambo ya kisasa na kinavutia mataifa mengine ikiwemo Zimbabwe ambayo ina mahusiano mazuri na Tanzania tangu enzi za Uhuru kuhamasika kuleta madini yake katika kiwanda hicho kwa ajli ya kusafishwa.

Akiwa nchini, Naibu Waziri wa Madini na Uendelezaji Migodi wa Zimbabwe na ugeni alioambatana nao atatembelea masoko ya madini na migodi ya wachimbaji wadogo na wakubwa wa madini ikiwemo mgodi wa almasi Mwadui mkoani Shinyanga, mgodi wa GGM pamoja na machimbo ya Nyarugusu mkoani Geita uendeshaji wa sekta hiyo kuanzia uchimbaji, uchenjuaji, usafishaji hadi uuzaji madini na kubwa zaidi namna ya kudhibiti utoroshaji madini.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Naibu Waziri wa Madini na Uendelezaji Migodi wa Zimbabwe, Dkt. Polite Kambamura (katikati) akisikiliza jambo alipotembelea kiwanda cha kusafisha dhahabu Mwanza akiwa ameambatana na ujumbe wa maafisa wawili kutoka nchini humo.
Naibu Waziri wa Madini Tanzania, Dkt. Steven Kiruswa akieleza namna Tanzania ilivyopiga hatua katika sekta ya madini hususani kudhibiti utoroshaji madini na hivyo kuvutia mataifa mengine kuja kujifunza.
Naibu Waziri wa Madini Tanzania, Dkt. Steven Kiruswa (kulia) akizungumza na ujumbe kutoka Zimbabwe ukiongozwa na Naibu Waziri wa Madini na Uendelezaji Migodi wa nchi hiyo, Dkt. Polite Kambamura.

No comments:

Powered by Blogger.