LIVE STREAM ADS

Header Ads

BAKWATA Mwanza waanza kutekeleza maagizo ya Sheikh Mkuu wa Tanzania

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Sheikh wa Mkoa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke (katikati) akiwahimiza viongozi wenzake wa dini kuhamasisha wananchi kujiandaa kuhesabiwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi tarehe 23 Agosti 2022.


Na Hellen Mtereko, Mwanza
Viongozi wa dini ya kiislamu mkoani Mwanza wametakiwa kuwahimiza waumini wa dini hiyo kujiandaa kuhesabiwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi inayotarajuwa kufanyika Agosti 23, 2022.

Sheikh wa Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke alitoa rai hiyo Juni 15, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za BAKWATA zilizopo Mbugani.

Alisema viongozi wa dini wakiwemo maimamu na wakuu wa taasisi za dini ya kiislamu wanao wajibu wa kuwaelimisha waumini wao kuhusu umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ambapo pia Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir Juni 10, 2020 akiwa ziarani mkoani Kagera aliwaelekeza Mashehe wote wa mikoa nchini kuhakikisha elimu hiyo inatolewa kwa waumini.

"Sisi Baraza Kuu la Waisilamu wa Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza kwa ushirikiano wa pamoja na viongozi wote tumepokea maagizo ya Mufti na tumeanza kuyatekeleza kwa kutoa mwongozo wa namna ya kufikisha elimu ya Sensa kwa waumini kupitia nyumba zetu za ibada" alisema Sheikh Kabeke.

Sheikh Kabeke alisema waumini wa dini ya kiislamu na wananchi kwa ujumla wanapaswa kuhesabiwa kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ili kupata Takwimu sahihi zitakazosaidia Serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine Sheikh Kabeke alisema Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir analaani vikali matukio ya ukatili yanayoripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya wanandoa kuuana.

Sheikh Kabeke alisema kutokana na hali hiyo ya mauaji katika jamii hususani kwa wanandoa, BAKWATA Mkoa wa Mwanza wamejipanga kuanzisha utaratibu wa kutoa mafunzo kwa wanandoa ya wiki mbili kabla ya kufunga ndoa.

"Tumetengeneza taratibu zote za mafundisho ili kuondokana na dhana ya kwamba ndoa ni jambo la anasa, fasheni au utamaduni na badala yake tufahamu kuwa ndoa ni jambo la dini na ibada" alisema Sheikh Kabeke.

No comments:

Powered by Blogger.