LIVE STREAM ADS

Header Ads

Chuo Kikuu CUHAS-Bugando chatoa Mafunzo kwa Wataalamu wa Afya Tanzania

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya utoaji huduma bora kwa wagonjwa wa dharura na mahututi yaliyohitimishwa katika Chuo cha CUHAS-Bugando jijini Mwanza tarehe 17 Juni 2022 wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mganga Mkuu Mkoa Mwanza, Dkt. Thomas Rutachunzibwa (wa nne kulia).
***
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wataalamu 180 wa sekta ya afya kutoka Hospitali za Rufaa 18 nchini wamepatiwa mafunzo kuhusu utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa mahututi na wale wa dharura.

Mafunzo hayo yameratibiwa na Wizara ya Afya kupitia fedha za Uviko 19 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) yameendeshwa kwa muda wa miezi miwili kwa makundi ya watu 60.

Mkurugenzi wa Mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya (CUHAS -Bugando), Profesa Jeremiah Seni amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa sababu Serikali pia imewekeza nguvu nyingi katika kujenga vitengo vya dharura, vyumba vya wagonjwa mahututi pamoja na kuweka vifaa tiba hivyo wataalamu wanahitajika kwa ajili ya kufanya kazi katika vituo hivyo.

Amesema kwa sasa kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa dharura na mahututi ikiwemo ajali za barabarani, kiharusi na mlipuko wa hivi karibuni wa ungonjwa wa UVIKO 19 hivyo kupitia mafunzo hayo wanajamii watakuwa na uhakika wa kupata matibabu bora.
"Mafunzo haya ni muhimu sana kwa madakitari,manesi na ninaimani kama tukiyatoa mara mbili kwa mwaka itakuwa ni njia nzuri ya kuwafikia watumishi wengi zaidi na kuleta tija katika kuokoa maisha ya watanzania",amesema Seni
Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa CUHAS-Bugando, Pro. Peter Rambau akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa chuo (CUHAS-Bugando), Prof. Peter Rambau ametoa shukurani kwa Wizara ya Afya kwa kuratibu mafunzo hayo ambayo yatachochea utoaji bora wa huduma kwa watanzania.

"Tunaiomba Wizara iendelee kufadhili mafunzo haya kwa sababu ni muhimu katika kuimarisha huduma za afya kwa jamii na kushauri CUHASI, Bugando kuwa Kituo rasmi cha kutoa mafunzo ya huduma za dharura" amesema Prof. Rambau.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Thomas Rutachunzibwa akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta ya afya katika utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa wa dharura na mahututi yaliyofanyika kwenye Chuo cha CUHAS-Bugando.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachunzibwa amesema wagonjwa wa dharura wanaanzia kwenye Zahanati Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya hivyo amewaasa washiriki wa mafunzo hayo kuweka utaratibu wa kuifikisha elimu waliyoipata kwenye ngazi za chini kwa kuangalia maeneo ambayo Serikali imefikisha vifaa tiba.

Naye mmoja wa washiriki wa Mafunzo hayo kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kigoma Maweni, Dkt. Ashraf Bitaliho amesema elimu waliyoipata itawasaidia kufanya kazi kwa weledi na ufanisi zaidi.

Kwa upande wa mshiriki mwingine kutoka Hospitali Maalumu ya Tiba ya Magonjwa Ambukizi Kibong'oto Kilimanjaro, Dkt. Anna Chongolo amesema mafunzo hayo ni muhimu na washiriki wameyapokea kwa mtazamo chanja kwani yatawasaidia huduma bora za Afya kwa jamii.

No comments:

Powered by Blogger.