LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Biteko atoa Wiki Moja kwa Wachimbaji kulipa madeni yao

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko ametoa wiki moja kwa wachimbaji wa mawe/ madini ya Chuma Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma kulipa madeni wanayodaiwa na wananchi wanaofanya kazi ya kuponda madini hayo.

Agizo hilo alilitoa Julai 04, 2022 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Asanje mara baada ya kutembelea maeneo ya wachimbaji wa chuma na kupokea malalamiko.

Dkt.Biteko alimwelekeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma kusimamia agizo hilo kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda ili wanachi hao wa Asanje walipwe fedha zao wanazowadai wawekezaji hao.

"Mhe Mkuu wa wilaya, kama kuna mtu atakuwa hajalipwa hadi jumatatu Afisa Madini unasimamisha mgodi huo mara moja bila masharti yoyote, uandike kabisa kwa maelekekeao ya Waziri nasimamisha" asisitiza Dkt. Biteko.

Aidha aliwataka wachimbaji wa madini na wawekezaji katika Sekta ya Madini kuhakikisha wanashirikisha wananchi katika mipango yao ya uwekezaji kabla hawajawekeza kwenye miradi hiyo ili kupunguza malalamiko yanayojitokeza mara kwa mara. Amesema, ushirishwaji utasaidia kujua vipaumbele vya wanachi ili iwe rahisi kwa utekelezaji.

"Nataka niwaambieni wenye leseni, leseni hizi mmepewa kwa niaba ya Watanzania wengine. Kwa kuwa tumewapa wenzetu leseni ya kuchimba matarajio ya Serikali ni kwamba hawawezi kugeuka tena kuwa kero kwa watu ambao wako maeneo ya kuchimba"alisema Dkt. Biteko.
Wilaya ya Bahi yanapatikana madini mbalimbali yakiwemo dhahabu, chuma na madini ujenzi.

Naye Mbunge wa Jimbo la Bahi, Kenneth Nolo alisema ziara ya Dkt.Biteko katika Kijiji cha Asanje kusikiliza malalamiko ya wanachi hao, imekuwa na manufaa kwa wananchi na matarajio makubwa katika shughuli za uchimbaji madini.

Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Munkunda alimshukuru Dkt.Biteko kwa kuweza kufika na kusikiliza changamoto za wananchi hao kwani ilikuwa ni kiu kubwa ya kuweza kufikisha malalamiko yao kwake.

No comments:

Powered by Blogger.