LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kamati ya Fedha jijini Mwanza yaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza imekagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya afya, elimu na ujenzi na kuridhishwa na usimamizi wa miradi hiyo.

Kamati hiyo ikiongozwa na Diwani wa Viti Maalum, Sikitu Sanziyote aliyemwakilisha Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine imekagua miradi hiyo Agosti 29, 2022 ikiwa ni kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha/ bajeti.

Miongoni mwa miradi iliyokaguliwa na Kamati hiyo ni pamoja na jenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Buhongwa, kiwanda cha kisasa cha kufyatua matofali Buhongwa, ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Ibanda, mradi mkubwa wa Kituo cha kisasa cha mabasi Nyegezi pamoja na ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika hospitali ya Wilaya Nyamagana, Butimba.

Akitoa taarifa mbele ya Kamati hiyo kuhusu ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Ibanda iliyopo Kata ya Mkolani, Mkuu wa shule ya Sekondari Mkolani na msimamizi wa shule hiyo mpya, Mwl. Joseph Maige alisema hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 96 na wanatarajia ifikapo Januari 2023 Shule ianze kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza wapatao 80.

"Shule hii itakapoanza kufanya kazi itapunguza msongamano katika shule zilizopo kwenye Kata ya Mkolani hususani katika Sekondari ya Mkolani ambayo inawatoto wengi, naamini watoto wakiwa wachache kwenye darasa watajifunza na kuelewa vizuri na walimu watapata wepesi wa kuwafundisha" alisema Mwl. Maige

Naye Diwani wa Kata ya Mkolani, Dioniz Swalala aliiomba Kamati hiyo kufanya jitihada za upatikanaji wa maji, umeme pamoja na samani za ofisi ili shule hiyo mpya ikamilike katika nyanja zote hatua itakayosaidia wanafunzi kusoma katika mazingira rafiki.

Kwa upande wake Sikiti Senziote aliyemwakilisha Meya Sima, alieleza kuridhishwa na usimamizi wa miradi waliyotembelea na kuongeza kuwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza itaendelea kusimamia vizuri miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, shule mpya, majengo ya kutolewa huduma za afya pamoja na Kituo cha Mabasi Nyegezi ili ikamilike na kutoa huduma kwa wananchi.

"Katika Shule hii mpya ya Ibanda tutajitahidi kukamilisha mahitaji yaliyopo ili hadi kufikia mwakani ianze kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza na kuondoa adha ya mrundikano uliopo Shule ya Sekondari Mkolani" alisema Senziote.
Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikikagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari Ibanda.
Mwonekano wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika Hospitali ya Wilaya Nyamagana, Butimba.
Mwakilishi wa Mstahiki Meya Jiji la Mwanza, Sikitu Sanziyote (kulia) akiwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Dkt. Pima Sebastian (kushoto) pamoja na wajumbe wa Kamati ya Fedha na Uongozi wakikagua jengo la wagonjwa wa nje katika Hospital ya Wilaya Nyamagana, Butimba.
Meneja mradi wa kiwanda cha tofali Cha Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Leonard Majuto (kulia) akitoa maelezo kuhusiana na usimamizi wa mradi huo.
Meneja mradi wa Kituo cha Mabasi Nyegezi, Mhandisi Henry Chundu (kulia) akitoa taarifa fupi ya maendeleo ya ujenzi wa Kituo hicho kwa Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Akizungumzia mradi wa Kituo cha mabasi Nyegezi, Meneja wa mradi huo Mhandisi Henry Chundu alisema ujenzi huo umegharimu zaidi ya bilioni 15 na umefikia asilimia 95 ambapo wanatarajia kuukabidhi Septemba 18, 2022.
Na Hellen Mtereko, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.