LIVE STREAM ADS

Header Ads

Makarani watakiwa kufanikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa weledi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
 Mkuu wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa wilayani humo, Remidius Mwema amewataka makarani, wasimamizi wa maudhui na Tehama kuzingatia mafunzo wanayopewa ili kufanikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.

Mwema aliyasema hayo Julai 31, 2022 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya makarani, wasimamizi wa Tehama na maudhui ambao watashiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi litakalofanyika nchini Agosti 23, 2022.

"Wewe uliye hapa utambue thamani kubwa uliyopewa na Serikali ya kushiriki zoezi hili kubwa la kitaifa ambalo linaenda kufanyika nchini kwetu, tambua hauko hapa kwa bahati mbaya" alisema Mwema.

Alisema zoezi la Sensa ni muhimu kwani husaidia kupanga mipango ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, barabara, afya na umeme hivyo kuzingatia kwao mafunzo hayo kutasaidia ukusanyaji wa taarifa sahihi za watu na makazi na kuirahisishia Serikali kupanga mipango yake ya kimaendeleo.

"Serikali inawategemea sana, usipozingatia mafunzo haya ukafanya mzaha utakua umeharibu taswira nzima ya zoezi hili kitaifa na si Kongwa tu hivyo nisingependa yatokee hayo" aliongeza Mwema.
Suala la nidhamu na weledi ni muhimu, najua wengine mnatofautiana umri na vyeo hivyo ni vyema kuheshimiana, kusikiliza kwa umakini na kujiepusha na vitendo vyote ambavyo viko kinyume na maadili" alisema Mwema.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walimhakikishia DC Mwema kuwa watazingatia mafunzo waliyopewa na kwamba wako tayari kuhesabiwa lakini pia kufanikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.

Mafunzo ya makarani, wasimamizi wa maudhui na Tehama yalianza Agosti 31, 2022 yakitarajiwa kufikia tamati Agosti 18, 2022 kote nchini ambapo kwa Wilaya ya Kongwa yamegawanywa katika vituo vinne ambavyo ni Kongwa, Kibaigwa, Mlali na Mkoka yakijumuisha Makarani 1,197, wasimamizi wa Tehama 22 na wasimamizi wa maudhui 24.
Ikumbukwe wilaya ya Kongwa ndiyo Wilaya pekee ambayo itakuwa na matukio makubwa mawili Agosti 23, 2022, mosi uwepo wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi na pili ni Mbio za Mwenge wa uhuru.
Na Maganga Gwensaga Dodoma

No comments:

Powered by Blogger.